ANKARA: Uturuki yaukosoa Umoja wa Ulaya
28 Oktoba 2007Waziri mkuu wa Uturuki Reccep Tayyip Erdogan ameukosa Umoja wa Ulaya kwa kutofanya mengi kukabiliana na wapiganaji wa chama cha kikurdi, Kurdistan Wokers´ Party, PKK.
Erdogan amesema mataifa ya Umoja wa Ulaya hayawakamati wala kuwafukuza wanachama wa chama cha PKK.
Uturuki mara kwa mara imezitaka nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zifanye juhudi zaidi dhidhi ya chama cha PKK, ambacho umoja huo unakichukulika kama kundi la kigaidi.
Waziri Erdogan aliyasema hayo baada ya mazungumzo baina ya Uturuki na Irak kumalizika bila mafanikio kuhusu mapendekezo ya Irak kutaka kuzuia mashambulizi ya wapiganaji wa PKK nchini Uturuki kutoka Irak.
Makamu wa rais wa Irak, Tarik al Hashimi akiieleza hali ilivyo amesema hali ni tete na hatari sana. Kuna shinikizo kubwa dhidi ya serikali ya Uturuki kutoka kwa Waturuki na jeshi, na kwa hiyo hali ni ngumu na ya hatari.
Uturuki imeonya kwamba haitavumilia mashambulizi zaidi katika eneo la mpakani na imepeleka wanajeshi wake katika eneo hilo.
Mamia ya watu wamefanya maandamano katika miji ya Uturuki kukilaani chama cha PKK na kutaka hatua zichukuliwe dhidhi ya chama hicho.