1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUkraine

Baerbock azuru kwa mara nyingine Ukraine

21 Mei 2024

Waziri wa Mambo za Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock ameelezea wasiwasi wake hii leo juu ya hali mbaya inayovikabili vikosi vya Ukraine katika uwanja wa vita mashariki mwa nchi hiyo.

Ukraine Kyiv 2024 | Rais Volodymyr Zelensky na Annalena Baerbock
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky akipeana mkono na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock aliyezuru Kyiv Mei 21, 2024Picha: Ukrainian Presidential Press Service/Handout/REUTERS

Baerbock ameonyesha mashaka hayo wakati wa ziara yake ambayo haikutangzwa nchini Ukraine. 

Katika ziara hiyo, Baerbock, pamoja na mambo mengine ameyatolea wito mataifa ya magharibi kuipatia Ukraine mifumo zaidi ya kujilinda angani. Ziara yake  inafanyika baada ya Urusi kuvurumishia droni Ukraine usiku mzima wa kuamkia Jumanne, katika mashambulizi yaliyowajeruhi baadhi ya wakaazi katika mkoa wa Kharkiv, mashariki mwa Ukraine.

Baerbock amesema hali nchini Ukraine kwa mara nyingine imezorota mno, katikati ya mashambulizi makubwa ya droni yanayofanywa na Urusi dhidi ya miundombinu na raia katika mkoa huo wa Kharkiv. Hii ni ziara za nane ya Baerbock nchini Ukraine tangu Urusi ilipomvamia jirani yake huyo Februari 2022.

Amesisitiza kwamba ili kuyakabili mashambulizi hayo, ni lazima Ukraine ikasaidiwa mifumo zaidi ya kujilinda angani.

Urusi yaishambulia Ukraine, Baerbock akianza ziara

Annalena Baerbock (mwenye koti la njano), pamoja na Waziri wa Nishati wa Ukraine katika mojawapo ya mitambo mikubwa zaidi ya nishati ya makaa ya mawe ya Ukraine.Picha: Jörg Blank/dpa/picture alliance

Muda mfupi tu kabla Baerbock hajawasili Ukraine, vikosi vya nchi hiyo vilisema vilidungua droni 28 kati ya 29 zilizotengenezwa Iran, ambazo zilirushwa na Urusi usiku wa jana.

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky alisema wiki iliyopita kwamba mashambulizi haya ya Urusi kwenye mkoa wa Kharkiv yanaweza kuwa ni wimbi la awali tu na pengine vikosi hivyo vimeunuia hasa mkoa huo wa pili kwa ukubwa nchini Ukraine.

Kulingana na gavana aliyewekwa na Moscow kusimamia mkoa huo siku ya Jumanne, wanajeshi wao hivi sasa wanadhibiti karibu nusu ya mji wa Vovchansk, ulioko karibu na mpaka wa Urusi na uliokuwa ukikaliwa na karibu watu 17,000 kabla ya vita hivi na ambao sasa ni kitovu cha mapigano.

Msemaji wa jeshi la Ukraine wakati huohuo ameliambia shirika la habari la serikali kwamba mapigano huko Kharkiv yameendelea katika mazingira magumu na yanabadilika sana, licha ya mapigano kupungua.

Ukraine zawadhihaki msaada wa magharibi

Msemaji wa Ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov amesema misaada kwa Ukraine haitabadilisha chochote kwenye uwanja wa vitaPicha: Mikhail Tereshchenko/TASS/dpa/picture alliance

Kremlin kwa upande wake imemjibu Baerbock kwa kusema hata kama misaada ya magharibi itaongezeka kwa kiasi gani, haitabadilisha udhibiti wa Urusi kwenye uwanja wa vita. Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov amesema, itabadilisha kidogo tu hali ilivyo. Na Rais wa Urusi Vladimir Putin anaamini kwamba utafika wakati ambapo Ukraine na washirika wake wataishiwa tu, ingawa Baerbock anasisitiza kwamba hiyo ni ndoto.

Taarifa za Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa kutoka mjini Geneva zimesema mapema leo kwamba zaidi ya watu 14,000 wameukimbia mkoa huo wa Kharkiv, tangu kuanza kwa mashambulizi ya Urusi Mei 10.

Mwakilishi wa Shirika hilo nchini Ukraine Jarno Habicht amesema watu wengine 189,000 bado wako ndani ya kilomita 25 ya mpaka na Urusi na kwa kiasi kikubwa wanakabiliwa na kitisho cha mashambulizi hayo.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW