Annan ahimiza uchaguzi wa amani Kenya
25 Februari 2013Annan, ambaye alisaidia kuikoa Kenya isitumbukie katika machafuko makubwa miaka mitano iliyopita, amesema nchi hiyo iko katika mkondo sahihi kufuatia machafuko ya baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 yaliyosababisha vifo vya watu zaidi ya 1,000 na kuwalazimu wengine takriban 600,000 kuyakimbia makazi yao. Amewakumbusha Wakenya kwamba nchi yao imesimama katika poromoko la kujiangamiza yenyewe, kuzingatia vurugu zilizotokea baada ya uchaguzi uliopita.
"Chaguzi lazima zifanyike kwa amani, uhuru na haki. Lazima zifanywe kwa mujibu wa sheria, kwa uadilifu na zionyeshe ari ya wananchi. Hapo ndipo umoja wa kitaifa, uthabiti na utangamano vitakapolindwa," amesema Annan katika taarifa yake.
"Matukio ya hivi karibuni ya machafuko na ongezeko la hali ya wasiwasi kuelekea uchaguzi, vinatia wasiwasi mkubwa sana. Kenya haiwezi kuhatarisha kurejea tena katika siku mbaya za huzuni, masikitiko na giza," akaongeza kusema Kofi Annan.
Annan amesaidia mchakato wa amani
Mapema mwaka 2008, Annan alisaidia kufikiwa muafaka wa kisiasa kati ya wagombea wawili wakubwa wa urais wakati huo. Makubaliano hayo yalimuwezesha Mwai Kibaki kubakia kuwa rais na mpinzani wake mkuu, Raila Odinga, akawa waziri mkuu. Kibaki hagombei wadhifa wowote katika uchaguzi ujao, kwa kuwa kisheria amekamilisha muda wake kama rais wa nchi, lakini Odinga ni miongoni mwa waombea wanane wanaowania kuingia ikulu.
Katika taarifa yake, Annan amewaasa Wakenya kuwa uchaguzi hautakiwi kuangaliwa kama shindano ambapo mshindi atachukua kila kitu. Amekumbusha kwamba Kenya ina katiba mpya na idara ya mahakama iliyoimarika. Ametaka matokeo ya uchaguzi huru na wa haki yaheshimiwe na mivutano yote itakayojitokeza, isuluhishwe mahakamani.
Annan amekuwa akizuru mara kwa mara nchini Kenya kukutana na maafisa wa ngazi za juu, akiwa na matumaini ya kusaidia kuepusha machafuko ya uchaguzi. Lakini katibu huyo mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa hajaitembelea Kenya kwa miezi kadhaa kwa sababu baadhi ya viongozi wa nchi hiyo waliziona ziara zake kama hatua ya kuyaingilia masuala ya ndani ya taifa hilo.
Kerry ataka uchaguzi usio na vurugu
Wakati huo huo, waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani, John Kerry, ametaka uchaguzi wa Kenya ufanyike kwa amani. Kerry amewahimiza Wakenya kufanya uchaguzi huru na wa haki bila kufanya machafuko. Ujumbe wake umewasilishwa kwa Wakenya wakati alipompigia simu rais wa Kenya, Mwai Kibaki.
"Nimezungumza na rais Kibaki. Sasa ni wakati wa Kenya kuungana pamoja, uchaguzi huru, wa haki na halali usio na machafuko – JK," wizara ya mambo ya kigeni imeandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter.
John Kerry ndiye afisa wa hivi karibuni wa cheo cha juu wa Marekani kuzungumzia uchaguzi wa Kenya, ambao umepangwa kufanyika Machi 4, 2013.
Mwandishi: Josephat Charo/APE
Mhariri: Bruce Amani