Annan amkazia sauti Assad
3 Juni 2012Annan , ambaye ameteuliwa kuwa mjumbe maalum nchini Syria na umoja wa mataifa pamoja na umoja wa mataifa ya Kiarabu, Arab League, amesema uwezekano wa kutokea vita vya wenyewe kwa wenyewe unakuwa mkubwa kila siku na kutia wasi wasi mataifa mengine ya mashariki ya kati.
Hali hiyo ya hofu , inaongezeka kutokana na kuuwawa kwa watu tisa na wengine 42 wamejeruhiwa katika mapigano kati ya watu wanaomuunga mkono Assad na wale wanaompinga ambao wameshambuliana kwa silaha kali na makombora katika nchi jirani ya Lebanon , katika mji wa bandari wa Tripoli.
Katika mkutano na viongozi wa umoja wa mataifa ya Kiarabu , Annan ametoa tathmini yenye kuonyesha hali isiyoridhisha nchini Syria miezi 15 tangu kuanza kwa vuguvugu la maandamano dhidi ya Assad na wiki moja baada ya mauaji ya zaidi ya watu 100 ambayo waangalizi wa amani wa umoja wa mataifa wanayalaumu majeshi ya rais Assad.
Assad ni lazima achukua hatua madhubuti zinazoonekana haraka kubadilisha msimamo wa majeshi yake na kutekeleza majukumu yake na kuondoa majeshi yake katika maeneo ya raia na kuacha matumizi yote ya nguvu dhidi ya raia, amesema Annan , ambaye amekutana na kiongozi wa Syria mjini Damascus siku ya Jumanne.
Kitu muhimu sio maneno anayotumia lakini hatua anazochukua hivi sasa, amesema mjumbe huyo maalum, na kuongeza kuwa ujumbe wake kwa Assad umekuwa , ni wa moja kwa moja na wa wazi.
Annan , ambaye amekuwa akizuru eneo hilo, amesema kuwa uwezekano wa kutokea vita vya wenyewe kwa wenyewe, na kuleta hofu ya kuzuka kwa mapambano ya kimadhehebu, inaongezeka kila siku.
Hisia zangu zinaambatana na wasi wasi wa nchi jirani ya Syria na nimezionyesha katika majadiliano yangu ya hivi karibuni.
Waziri mkuu wa Lebanon Najib Mikati amekwenda haraka mjini Tripoli kiasi ya kilometa 70 kaskazini mwa Beirut , kujaribu kuzuwia ghasia katika eneo hilo. Jeshi limeingia katika eneo hilo likiwa na magari ya deraya lakini hayakufyatua risasi.
Vifo vilivyotokea siku ya Jumamosi ni idadi ya juu kabisa katika siku moja mjini Tripoli, na kuzusha hofu kuwa ghasia nchini Syria zinaweza kusambaa hadi katika nchi hiyo jirani.
Mwandishi : Sekione Kitojo /rtre
Mhariri: Sudi Mnette