1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Annegret Kramp-Karrenbauer amrithi Merkel uongozi wa CDU

Daniel Gakuba
7 Desemba 2018

Annegret Kramp-Karrenbauer alikuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, akiwa mshirika wa karibu wa Kansela Angela Merkel. Lakini kabla ya kura kupigwa, aliwaambia wajumbe wa chama kwamba yeye ni mtu huru.

Deutschland CDU-Parteitag in Hamburg Kramp-Karrenbauer und Merkel
Picha: Reuters/K. Pfaffenbach

Katika uchaguzi uliofanyika kwenye kikao cha chama cha Christian Democratic Union mjini Hamburg, muda mfupi uliopita Annegret Kramp-Karrenbauer amepata asilimia 51 ya kura katika duru ya pili ambapo amapambana na Friedrich Merz. Mgombea wa tatu, waziri wa afya wa sasa Jens Spahn alienguliwa katika duru ya kwanza.

Akizungumza katika mkutano huo kabla ya uchaguzi kufanyika, Bi Kramp-Karrenbauer amesema anaelewa dhana iliyopo kwamba yeye ni Merkel-mdogo, akasisitiza kwamba yeye siyo nakala ya Merkel, na kwamba anasimama kama mtu huru.

Annegret Kramp-Karrenbauer, mwenyekiti mpya wa chama cha Christian Democratic Union - CDU.Picha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Mama huyu ambaye awali alikuwa Waziri Kiongozi wa jimbo la Saarland Kusini Magharibi mwa Ujerumani, alikuwa akiungwa mkono na Kansela Merkel katika uchaguzi huu. Tangu Februari mwaka huu, alikuwa Katibu Mkuu wa CDU.

Mshikamano ndani ya chama

Chumba cha mkutano kiliripuka kwa furaha yalipotangazwa matokeo ya uchaguzi. Kramp-Karrenbauer aliyetokwa na machozi ya furaha amewashukuru wapinzani wake, na kuwaalika kusimama naye jukwaani kama ishara ya mshikamano katika chama.

Awali, Angela Merkel alitoa hotuba ya kuaga uongozi wa chama chake akiwa mwingi wa hisia, akisema ''ilikuwa fahari kubwa kwangu, na imekuwa heshima kubwa.''

Kramp-Karrenbauer amejitofautisha kimsimamo na Merkel katika sera za kijamii na za uhusiano wa nje, kwa kuunga mkono sheria ya kuweka kiwango cha wanawake katika bodi za makampuni, na kuonyesha mtazamo mkali zaidi kuhusu Urusi. Wikim iliyopita aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba anaunga mkono Marekani na Ulaya kushirikiana kuzizuia meli za Urusi kuhusiana na mzozo wa Ukraine.

Ahueni kwa Angela Merkel

Kramp-Karrenbauer akiwa na wagombea aliowashinda, Jens Spahn (kushoto) na Friedrich Merz.Picha: Reuters/K. Pfaffenbach

Hata hivyo, kuhusiana na dira ya chama chake cha CDU, Kramp-Karrenbauer amesema hana jipya. Wakati wa kampeni alichukua msimamo wa tahadhari kuhusiana na mustakabali wa Ulaya kuliko mpinzani wake mkuu, Friedrich Merz, aliyesema kuwa Ujerumani inapaswa kuchangia zaidi katika umoja huo, kwa sababu uchumi wake unafaidika ikiwa uchumi wa ukanda wa sarafu ya euro uko imara.

Kuchaguliwa kwa Kramp-Karrenbauer ni kuidhinisha sera inayokibakisha  chama cha CDU katika mrengo jumuishi na wa kati, kuliko kurudi katika ule wa awali wa kihafidhina zaidi unaodhibitiwa na wanaume, ambao ulitakiwa na Merz.

Ingekuwa vigumu kwa Angela Merkel kuumaliza muhula wake wa ukansela hadi mwaka 2021 kama mpinzani wake Friedrich Merz angeshinda uongozi wa chama, ikitiliwa maanani kwamba misimamo yao inakinzana vikali.

Mradi sasa mgombea ambaye ni chaguo lake amechukua hatamu za chama, siku za mwisho za Bi Merkel kisiasa zitamalizika kwa utaratibu usio na mivutano.

 

Mwandishi: Daniel Gakuba/rtre, afpe

Mhariri: Mohammed Khelef

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW