1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guterres: Aomba Somalia na Ethiopia wasuluhishe tofauti zao

21 Januari 2024

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito kwa Somalia na Ethiopia kuanza mazungumzo ya kusawazisha mgogoro wao juu ya mpango wa Ethiopia na jimbo lililojitenga la Somaliland.

Antonio Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres Picha: Brendan McDermid/REUTERS

Akizungumza mjini Kampala anakohudhuria mkutano wa kilele wa G77 pamoja na China, Guterres amesema kupitia mazungumzo ndiko kutakapopatika suluhu ya mzozo uliopo. 

Wasiwasi umeonekana katika pembe hiyo ya Afrika tangu nchi isiokuwa na bahari ya Ethiopia kuwa na makubaliano na Somaliland mnamo Januari mosi  yanayoipa Ethiopia nafasi ya kutumia bahari ya shamu na badala yake nchi hiyo ilitambue  jimbo hilo kama taifa huru. 

Siku ya Alhamisi Somalia iliondoa uwezekano wa aina yoyote wa kuwa na mazungumzo na Ethiopia hadi pale makubaliano hayo yatakapofutwa na kuapa kupambana kuupinga. 

Somalia yasema hakuna nafasi ya upatanishi kati yake na Ethiopia

Kwengineko rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi amesema nchi yake haitokubali kitisho chochote dhidi ya Somalia au usalama wake, baada ya Ethiopia kusema itazingatia kutambua madai ya uhuru wa Somaliland.  

Katika mkutano na waandishi habari mjini Cairo akiwa pamoja na rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud, al Sisi amesema hatua ya taifa fulani kutaka kurukia ardhi ya watu na kutaka kuidhibiti ni kitu ambacho hakuna atakayekubaliana nacho. 

Somaliland ilijitangaza kuwa huru kutoka Somalia mwaka 1991 lakini bado haijatambuliwa na hata nchi moja duniani kuwa nchi huru. 
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW