1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMamlaka ya Palestina

Antony Blinken asema hali ya Gaza inazidi kuwa mbaya

19 Machi 2024

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Antony Blinken, amesema watu wa Gaza wanapitia kipindi kigumu cha ukosefu wa chakula, huku akielezea umuhimu wa kufikisha misaada ya kibinaadamu katika eneo zima la Palestina.

Marekani | Antony Blinken
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Antony Picha: Olivier Douliery/AP Photo/picture alliance

Antony Blinken amesema asilimia 100 ya watu wa Gaza wapo katika viwango vya juu vya ukosefu wa chakula na wanahitaji msaada wa haraka.  Amesema bado dunia inaendelea kushuhudia hali mbaya inayotisha ya kibinaadamu kwa watoto, wanawake na wanaume.

Kauli hiyo ya Antony Blinken imekuja siku moja kabla ya kurejea Mashariki ya Kati, safari hii akiwa Saudi Arabia na Misri kujadili mipango ya kuwa na makubaliano ya kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza ili kutoa nafasi ya misaada zaidi kuingizwa katika eneo hilo linalokabiliwa na vita.

UN: Nusu ya wakaazi wa Gaza wanakabiliwa na baa la njaa

Siku ya Jumatatu Umoja wa Mataifa ulionya kuwa nusu ya watu wa Gaza wanakabiliwa na baa la njaa na kukadiriwa kufikia kiwango kibaya mwezi Mei, iwapo hatua za haraka hazitochukuliwa. Mkuu wa shirika la misaada la Umoja huo Martin Griffiths ameitolea mwito Israel kukubali misaada zaidi kuingia katika eneo lililozingirwa la Palestina akisema muda haupo tena na watu wanahitaji chakula.

Uingereza yatoa wito wa mapigano kusitishwa kwa muda

Naibu Waziri Mkuu wa Uingereza Oliver Dowden, atoa wito wa kusitishwa mapigano kwa muda ili misaada ya kiutu iweze kufikishwa mjini Gaza. Picha: Ismael Mohamad/UPI Photo/IMAGO

Kwengineko Naibu Waziri Mkuu wa Uingereza Oliver Dowden, amesema anatetea haki ya Israel ya kujilinda kufuatia mivutano iliyopo kati ya taifa hilo na baadhi ya washirika wake, lakini pia akatoa wito wa kusitishwa mapigano kwa muda ili misaada ya kiutu iweze kufikishwa mjini Gaza. Mwanadiplomasia huyo wa Uingereza amesema nchi yake mara zote imekuwa ikiiomba Israel kuzingatia sheria ya kibinaadamu ya kimataifa na pia kutaka misaada ipelekwe Gaza.

Hapo jana Rais wa Marekani Joe Biden alimuonya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kwamba operesheni ya ardhini anayopanga kufanya katika mji wa Rafah, itafanya hali kuwa mbaya zaidi Gaza na kukubaliana kwamba timu ya mataifa yote mawili zitakutana leo  mjini Washington kujadili suala hilo.

Israel yaidhinisha operesheni ya kijeshi Rafah

Huku hayo yakiarifiwa, wapalestina 20 wameuwawa leo Jumanne katika mashambulizi ya angani mjini Rafah na katika maeneo mengine ya Ukanda wa Gaza.

Kulingana na maafisa wa afya wa ukanda huo, watu 14 wameuwawa wakati makombora yalipofurumishwa katika majumba yao na wengine 6 wameuwawa katika shambulizi la angani lillofanywa katika kambi ya wakimbizi ya Al Nuseirat. Miezi takriban sita ya mapigano kati ya Israel na wanamgambo wa Hamas mjini Gaza na viunga vyake yamesababisha mauaji ya zaidi ya wapalestina 31,819 huku watu 73,934 wakijeruhiwa tangu kuanza kwa mapigano hayo Oktoba 7.

ap/afp/reuters