1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yasaka suluhu mzozo wa Mashariki ya Kati mjini Riyadh

Hawa Bihoga
9 Oktoba 2024

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi amewasili Riyadh, nchini Saudi Arabia siku ya Jumatano kuangazia juhudi za kumaliza oparesheni za jeshi la Israel katika maeneo ya Gaza na Lebanon.

Mashariki ya Kati | Abbas Araghtschi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi akiteremka katika ndegePicha: Iranian Foreign Ministry via AP/picture alliance

Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia Mwanamfalme Faisal bin Farhan amemmlaki Araghchi na ujumbe wake mjini Riyadh.

Awali msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran Esmail Baghaei aliandika katika mtandao wa X kwamba ziara ya kiongozi huyo itajikita katika kile alichokiita kukomesha "mauaji ya kimbari na uchokozi wa utawala wa Israel" na "kupunguza machungu na mateso ya raia wa Gaza na Lebanon."

Ziara ya mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu nchini Iran inafanyika katika wakati ambapo eneo lote la mashariki ya kati likiwa katika hali ya wasiwasi baada ya Israel kusema itajibu shambulizi la makombora la Iran katika ardhi yake juma lililopita.

Baghaei alisema kwamba mikutano ya Riyadh ni muendelezo wa juhudi za kidiplomasia kwa uratibu wa nchi za eneo hilo.

Wakati hayo yakiendelea wizara ya afya inayoongozwa na Hamas katika Ukanda wa Gaza imesema idadi ya Wapalestina waliouwawa tangu kuzuka kwa vita vya Gaza imepindukia elfu arobaini na mbili huku wengine 97,720 wakijeruhiwa.

Soma pia:Hizbullah yasema inaunga mkono usitishaji vita Lebanon

Hata hivyo idadi hiyo haijatofautisha kati ya raia na wapiganaji lakini Umoja wa Mataifa inazichukulia takwimu hizo kuwa ni za kuaminika.

Mapema siku ya Jumatano wakaazi wameripoti kuwa idadi kubwa ya watu wameuwawa na wengine wakijeruhiwa katika oparesheni za kijeshi za Israel hivi karibuni kaskazini mwa Ukanda wa Gaza.

Maeneo ambayo yaliathirika zaidi katika mashambulizi hayo ni pamoja na wilaya ya Shejaiya na kambi za wakimbizi za Jabalia na Nuseirat.

Nchini Israel wahudumu wa dharura wamesema watu wawili wameuwawa kwenye mji wa kaskazini wa Kiryat Shmona, kufuatia mapigano kati ya Israel na wanamgambo wa Hezbollah wa Lebanon.

EU: Tumeunda njia salama za anga kufikisha misaada Lebanon

Kuongezeka kwa mashambulizi kumesababisha mzozo mbaya wa kiutu hasa nchini Lebanon. Kufuatia hali hiyo, Umoja wa Ulaya umezindua kile ilichokiita "ukanda salama wa angani" kwa ajili ya kufikisha misaada ya kibinadamu nchini humo.

Msemaji wa Tume ya umoja huo Balazs Ujvari amesema safari tatu za awali za ndege tayari zimepangwa na ndege ya kwanza inatarajiwa kuwasili Ijumaa.

Israel yadaiwa kuishambulia Iran

01:17

This browser does not support the video element.

Hii inafuata juu ya kiasi kikubwa cha msaada cha dawa na vifaa vya matibabu ambavyo Umoja wa Ulaya umetuma kupitia utaratibu wa ulinzi wa raia wa umoja huo katika siku zilizopita.

"pia tumeongeza mgao wetu wa misaada ya kibinadamu kwa Lebanon zaidi ya Euro milioni 100 mwaka huu." Alisema Ujvari

Soma pia:Israel yaanzisha operesheni ya ardhini Lebanon, Iran yaionya kutoijaribu

Israel imezidisha mashambulizi kwenye kile ilichokiita ngome za Hezbollah nchini Lebanon tangu Septemba 23 na kusababisha vifo vya watu zaidi ya elfu moja na kulazimisha wengine zaidi ya milioni moja kuyakimbia makaazi yao.

Wakati huo huo Hamas imesema imeanza mikutani na kundi  hasimu la Fatah mjini Cairo kujadili vita vya Gaza pamoja na juhudi za kujenga umoja wa kitaifa.

Taarifa ya kundi hilo imesema wajumbe wa Hamas na Fatah walikuwa wanajadili uvamizi dhidi ya Gaza, matukio ya kisiasa na kuunganisha juhudi za kitaifa na safu.