Arbeloa: Mbappé lazima ajitoe uwanjani
13 Mei 2026
"Je, Mbappé atacheza Alhamisi dhidi ya Oviedo? Tutaona kama atamaliza mazoezi ya leo Jumatano, kwa sababu jana alifanya mazoezi. Kama atakuwa tayari, bila shaka atapata dakika za kucheza ili kuendelea kuonyesha kujitoa kwake kwa klabu yetu, na kucheza mechi tatu zilizobaki licha ya kuwa na kadi nne za njano. Kadi ya tano itamfanya asimamishwe,” alisema Alvaro Arbeloa katika mkutano na waandishi wa habari.
"Kama mshabiki wa Madrid kabla hata ya kuwa kocha, ningependa kumuona akiendelea kufanya kile anachokijua vizuri zaidi: kufunga mabao,” aliongeza kocha huyo kuhusu mfungaji wake bora, ambaye hakuwapo Jumapili katika Clasico iliyopotezwa dhidi ya FC Barcelona kwa sababu bado hakuwa amepona asilimia mia moja kutokana na majeraha ya misuli ya nyuma ya paja.
Kutokuwepo kwa Mbappé katika mechi hiyo, ambayo iliifanya Barcelona kutawazwa rasmi mabingwa wa Uhispania huku Real Madrid ikikosa taji lolote msimu huu, kumechochea tena mijadala nchini Uhispania kuhusu tabia yake inayotajwa kuwa ya ubinafsi.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Paris Saint-Germain amekosolewa vikali katika siku za hivi karibuni baada ya safari yake kwenda Sardinia mwishoni mwa wiki iliyopita wakati wachezaji wenzake walikuwa na mechi ya La Liga dhidi ya Espanyol Barcelona.
Baadhi ya mashabiki waliokerwa na mwenendo wake wamefikia hatua ya kutaka aondoke kupitia mitandao ya kijamii. Wengine walimlaumu kwa kuondoka katika kituo cha mazoezi akiwa anatabasamu Alhamisi iliyopita, mara tu baada ya mzozo mkali kati ya Aurélien Tchouaméni na Federico Valverde.
"Ni klabu yenye afya nzuri, inaongozwa vizuri na ina wachezaji wakubwa"
Arbeloa alipoulizwa kuhusu matumizi ya neno "kujitoa” katika jibu lake la kwanza, alifafanua kuwa anaamini Mbappé "amekuwa akijituma kwa asilimia mia moja kila wakati,” kwa sababu vinginevyo asingejua "mahali alipo.”
Mwandishi mmoja alipomuuliza kama Real Madrid "imefikia mwisho mbaya kabisa,” baada ya kauli tata ya rais wa klabu Florentino Pérez aliyelalamikia kampeni inayodaiwa kuendeshwa na vyombo vya habari pamoja na baadhi ya mashabiki dhidi yake, beki huyo wa zamani wa kulia alijibu:
"Hakuna klabu inayoweza kushinda Ligi ya Mabingwa Ulaya na La Liga kila mwaka. Sielewi kwa nini watu wanazungumzia kutokuwepo kwa utulivu ndani ya klabu au wachezaji kutokuwa na umoja. Real Madrid imekuwa ikifanya mambo vizuri kwa muda mrefu sana. Ni klabu yenye afya nzuri, inaongozwa vizuri na ina wachezaji wakubwa.”
"Nina uhakika msimu huu wa kiangazi klabu itafanya tathmini muhimu ili kuimarisha kikosi na kuifanya Madrid irudi ikiwa na nguvu zaidi. Kwa tafakari na kiwango cha juu kinachohitajika, Real Madrid itashinda tena, nina hakika,” Arbeloa alisisitiza.