1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nani atabeba Kombe la Copa America?

4 Julai 2015

Baadaye leo usiku, taji la Amerika Kusini hakitakuwa kitu pekee kitakachogombaniwa wakati Argentina na Chile zitakapokutana katika fainali ya dimba la Copa America leo usiku

Copa America 2015 Argentinien gegen Paraguay
Picha: GettyImages/AFP/Y. Cortez

Watani hao wa kikanda, wana fursa ya kuizika miaka mingi ya fedheha kwa kushinda mpambano huo utakaochezwa uwanja wa kitaifa wa Santiago. Wenyeji Chile hawajawahi kushinda taji la bara la Amerika ya Kusini, wakati Argentina ikimaliza miaka 22 bila kupata taji lolote kuu.

Mshindi atasherekea mafanikio makubwa ya kihistoria. Atakayeshindwa atabaki akijiuliza ni lini ataendelea kusubiri hadi atakapolinyanyua kombe hilo.

Wenyeji Chile wanalenga kushinda taji la Copa America kwenye ardhi ya nyumbaniPicha: Reuters

Ushindi kwa Argentina utakuwa jambo la ziada maalum kwa Lionel Messi, ambaye amenawiri katika klabu ya Barcelona kwa miaka mingi lakini hajawahi kuipa timu yake sababu yoyote cha kushangilia. Ikiwa Messi hatimaye ataliongoza taifa lake kutwaa taji hilo, atakuwa amewanyamazisha wakosoaji wake wengi wanaosema kuwa hajawahi kuichezea vyema timu ya taifa kama anavyofanya katika klabu ya Barca. Huyu hapa kocha wa Argentina Gerardo Martino

Argentina ilikaribia kutwaa taji kuu wakati ilifika fainali ya Kombe la Dunia nchini Brazil mwaka jana, na ikashindwa moja bila na Ujerumani katika muda wa ziada. Iliondolewa katika robo fainali ya kombe la dunia 2006 na 2010. Wargentina walipoteza fainali za Copa America 2004 na 2007.

Chile ina mojawapo ya vizazi vyake bora zaidi vya wachezaji. Kocha Muargentina Jorge Sampaoli anaongoza kikosi kinachowajumuisha wachezaji wa Juventus Arturo Vidal na Mauricio Isla, mshambuliaji wa Arsenal Alexis Sanchez, mshambuliaji wa Napoli Eduardo Vargas, kiungo wa Inter Milan Gary Medel, kiungo mshambuliaji wa Fiorentina Matias Fernandez na Jorge Valdivia wa Palmeiras. Huyu hapa Sampaoli

Chile ilifika 16 za mwisho katika Kombe la Dunia mwaka jana, kabla ya kuondolewa na wenyeji Brazil kwa mikwaji ya penalty. Hii ni fainali yake ya kwanza ya Copa America katika kipindi cha miaka 28.

Peru iliizaba Paraguay magoli mawili kwa sifuri na kuhakikisha kuwa wanamaliza katika nafasi ya tatu kwa mara ya pili mfululizo kwenye dimba hilo baada ya kumaliza ya tatu mwaka wa 2011

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Yusuf Saumu