Argentina yalipa kisasi kwa Ujerumani
4 Septemba 2014Ushindi huo mnono wa Argentina ni katika kile kinachoonekana ni kulipa kisasi baada ya kupoteza mchezo wa fainali ya kombe la dunia nchini Brazil mwaka huu.
Argentina ilikuwa tayari iko mbele kwa mabao 4-0 baada ya dakika 50 na kuzima sherehe za ubingwa wa dunia katika mchezo wa kwanza wa Ujerumani tangu kushinda kombe hilo kwa bao 1-0 dhidi ya Argentina mwezi Julai nchini Brazil.
"Haiwezi kuwa kulipiza kisasi," amesema kocha wa Ujerumani Joachim Loew. "Huwezi kurejesha fainali tena."
Wakati Lionel Messi hakuwapo uwanjani kutokana na maumivu ya mguu wake wa kulia , Di Maria alichukua jukumu la kuiongoza safu ya ushambuliaji ya Argentina jana , alimmegea Sergio Aguero pasi safi katika dakika ya 21, EriK Lamela aliweka mpira wavuni katika dakika ya 40 na Federico Fernandez alipachika goli la tatu kwa kichwa dakika mbili baada ya kipindi cha pili kuanza.
Di Maria ang'ara
"Angel di Maria alionesha kwa nini ni mmoja kati ya wachezaji watano wazuri duniani," amesema kocha wa Argentina Gerardo Martino.
Andre Schuerrle alipunguza idadi ya magoli dakika mbili kabla ya Mario Goetze kupachika bao la pili kwa Ujerumani usiku huo na kumaliza mchezo huo , Ujerumani ikiwa nyuma kwa mabao 4-2.
Hata hivyo Ujerumani ilifanya mabadiliko makubwa katika kikosi chake kwa kuwachezesha vijana chipukizi.
Nahodha Philip Lahm , mlinzi wa kati Per Mertesacker na mshambuliaji anayeshikilia rekodi ya kufunga mabao mengi katika michezo ya fainali za kombe la dunia kwa sasa Miroslav Klose wote wamestaafu baada ya fainali hiyo nchini Brazil.
England bado yasua sua
Hamasa ya kuanza vizuri kwa kikosi cha Uingereza haikupata chachu katika uwanja wa wembley jana licha ya nahodha mpya wa kikosi hicho Wayne Rooney kuanza kazi yake hiyo mpya kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Norway baada ya kuifungia timu yake mkwaju wa penalti jana.
Kwa mara ya kwanza katika historia ya miaka saba ya uwanja uliofanyiwa ukarabati wa hali ya juu wa Wembley , uwanja huo ulikuwa una mashabiki nusu uwanja tu kwa mchezo wa kimataifa wa Uingereza, wakati mashabiki 40,181 wakishuhudia hali ile ile ya kusuasua ya kikosi cha Uingereza.
Mapambano mengine ni kati ya Marekani na jamhuri ya Czech , ambapo US Boys walipata ushindi wa bao 1-0 mjini Prahue.
Denmark ikaangukia pua mbele ya Uturuki kwa kufungwa mabao 2-1 mjini Kopenhagen , Ukraine ikailaza Moldova kwa bao 1-0 na Urusi ikaizaba Azerbaijan kwa mabao 4-0. Jamhuri ya Ireland ikaiangusha Oman kwa mabao 2-0.
Mwandishi : Sekione Kitojo / rtre / ape