1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Argentina yatinga fainali Kombe la Dunia

14 Desemba 2022

Mbichi na mbivu zimeshajuilikana kwenye Kombe la Dunia kwa Lionel Messi kumtimua Luka Modric kwenye kinyang'anyiro hicho na sasa Argentina inangojea kuminyana na ama Moroko au Ufaransa kwenye fainali.

WM Katar 2022 | Halbfinale | Argentinien vs. Kroatien
Picha: Natacha Pisarenko/AP Photo/picture alliance

Yalikuwa ni magoli mawili yaliyowekwa kimiani na mshambuliaji Julian Alvarez, yakitanguliwa na mkwaju wa penalti kutoka kwa Messi uliotingisha nyavu za Croatia  katika dakika ya 39 vilivyozusha shamrashamra na sherehe si uwanjani Lusail tu mjini Doha, bali kote nchini Argentina, ambako maelfu ya mashabiki wamejitokeza mitaani kumtukuza shujaa wao, Messi, kwa kuiongoza timu yao ya taifa kwa ushindi wa 3-0 dhidi ya Croatia na hivyo kujikatia tiketi ya moja kwa moja kuelekea fainali. 

Je, Croatia itaweza kumzuia nyota wa Argentina Lionel Messi?

This browser does not support the audio element.

Kwa ujumla, mechi hii inatajwa kuwa miongoni mwa zile bora kabisa kushuhudiwa kwenye Kombe la Dunia mwaka huu.

Kwa wengi, mchezo huu ulikuwa fursa ya mwisho ya Messimwenye umri wa miaka 35 sasa kuthibitisha uwezo wake na pengine kutimiza ndoto yake ya kuja kubeba kombe hilo la juu kabisa katika ulimwengu wa soka. 

Baada ya mechi hiyo, Messi aliwaambia waandishi wa habari kwamba moyo wake umejaa mchanganyiko wa furaha na hamasa kuwaona wale aliowaita familia yake, akimaanisha mashabiki, "wakipeperusha bendera za nchi yao kwa furaha ya ushindi."

"Muhimu kuliko yote ni kwamba sasa tunakwenda kwenye fainali na hicho ndicho hasa tulichokuwa tunakitaka." Alisema nahodha huyo wa Argentina.

Fainali ya mwisho kwa Messi?

Lionel Messi (kushoto) na Julian Alvarez, wafungaji wa Argentina kwenye nusu fainali na Croatia tarehe 13 Disemba 2022.Picha: Martin Meissner/AP Photo/picture alliance

Hii itakuwa fainali ya pili na pengine ya mwisho kwa Messi kwenye Kombe la Dunia, baada ya ile ya mwaka 2014, ambapo Argentina ilibwagwa na Ujerumani.

Wachambuzi wa soka wanasema ni kama kwamba jukwaa linatayarishwa kumuaga Messi akiwa katika kilele cha mafanikio yake kwenye ulimwengu wa kabumbu.

Hata goli la tatu lililowekwa kimiani katika dakika ya 69 na mshambuliaji Alvarez lilitokana na pasi maridadi kabisa iliyotoka kwa Messi baada ya kuwala chenga Wakroatia, akiwamo Josko Gvardiol, anayetajwa kuwa mmoja wa walinzi bora kabisa kwenye Kombe la Dunia mwaka huu.

Messi amebeba jukumu la kuingoza Argentina kutwaa Kombe la Dunia kwa mara ya tatu, mwenyewe akiwa amefunga katika mechi tano kati ya sita walizocheza nchini Qatar.

"Ni jambo la heshima kubwa kwangu kumfunza na kumuona akicheza. Kila unapomuona unajuwa kuwa yeye ni chanzo kikubwa cha hamasa kwa wachezaji wenzake, mashabiki na dunia nzima." Alisema kocha wake, Lionel Scaloni, baada ya mchezo huo.

Mwisho wa Modric kwenye Kombe la Dunia 

Lionel Messi (kulia) akifunga goli la kwanza kati ya matatu dhidi ya Croatia katika nusu fainali ya Kombe la Dunia tarehe 13 Disemba 2022.Picha: Tom Weller/dpa/picture alliance

Kwa upande wa Croatia, hii ni mara ya pili kushindwa kuingia kwenye fainali, licha ya kuzibwaga Japan na Brazil katika hatua ya mtoano.

Kwa nyota wake, Luka Modric, mwenye umri wa miaka 37, huenda hii ikawa mechi yake ya mwisho kwenye Kombe la Dunia.

Nyota huyo alilazimika kubadilishwa katika dakika ya 89 huku akiwa na pua nyekundu kutokana na mpira uliompiga usoni mapema kwenye mechi hiyo ngumu sana kwake.

Kocha wa Croatia alikiri kwamba walianza kuupoteza mchezo tangu mwanzo. "Goli la kwanza liliuchukuwa mchezo mzima na kuuelekeza kwengine. Alikuwa ni yule Messi hasa ambaye sote tulitarajia kumuona." Alisema.

Argentina imedumisha rikodi yake ya kutokupoteza kwenye nusu fainali na sasa inafikia hatua ya fainali kwa mara ya sita.