Armenia na Azerbaijan zalumbana upya
20 Juni 2024Armenia na Azerbaijan zimelumbana upya kwa maneno makali jana Jumatano baada ya Ufaransa kuahidi kuipelekea silaha mpya Armenia.
Nchi hizo mbili katika eneo la Caucasus Kusini zimepania kupiga hatua miezi ya hivi karibuni katika utekelezaji wa mkataba wa amani unaojumuisha uwekaji wa mipaka, huku Armenia ikikubali kukabidhi vijiji vinne vya mpakani vinavyozozaniwa kwa Azerbaijan.
Tangazo la Jumanne wiki hii la waziri wa ulinzi wa Ufaransa Sebastien Lecornu kwamba Ufaransa ingeiuzia silaha Armenia limezua ukosoaji mkali kutoka kwa Azerbaijan.
Soma pia: Kiongozi wa Armenia asema mkataba wa amani na Azerbaijan wakaribia
Hikmet Hajiyev, mshauri wa cheo cha juu wa sera ya kigeni kwa rais wa Azerbaijan Ilham Aliyev ameviambia vyombo vya habari vya Azerbaijan kwamba hawaichukulii sera ya Ufaransa katika eneo la Caucasus Kusini kuwa na tija na ni sera mbaya yenye madhara.
Hajiyev amesema sera hiyo ni pigo kwa mahusiano kati ya Azerbaijan na Armenia.