1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Armenia na Azerbaijan zatumbukia kwenye mapigano mapya

Admin.WagnerD14 Oktoba 2020

Vikosi vya Armenia na Azerbaijan vimetumbukia kwenye mapigano mapya ya kuwania udhibiti wa jimbo la Nagorno Karabakh licha ya miito ya kusitisha mapigano na kuanzisha mazungumzo ya kutatua mzozo huo.

Aserbaidschan | Berg-Karabach | Stepanakert
Picha: Aris Messinis/AFP/Getty Images

Shirika la Habari la AFP limeripoti mashambulizi makali ya mabomu kwenye wilaya ya Terter na mtambo wa kufyetua makombora wa Azerbaijan umeonekana ukijitayarisha kuyapiga maeneo ya milimani.

Viongozi wa vuguvugu la wanaotaka kujitenga kwa jimbo la Nagorno Karabakh wameilaumu Azerbaijan kwa kuanzisha mashambulizi kwenye maeneo kadhaa ya jimbo hilo.

Azerbaijan nayo kwa upande mwingine imeituhumu Armenia kwa kufyetua makombora kwenye wilaya za Goranboy, Terter na Agdam zilizopo nje kidogo ya jimbo la Karabakh.

Mapigano ya zaidi ya wiki mbili kati ya Armenia na Azerbaijan yamesababisha vifo vya watu 600 ikiwemo raia 73, idadi ambayo ni jumla ya tarakimu zilizotolewa na kila upande.

Shirika la Msalaba Mwekundu latahadharisha kuhusu athari za mapigano

Picha: Umit Bektas/Reuters

Shirika la Msalaba Mwekundu limesema hadi sasa maelfu ya watu wameathirika na mzozo wa kuwania Nagorno Karabkh.

Mkuu wa shirika hilo kwa kanda ya Ulaya na Asia Martin Schuepp ametahadharisha juu ya mzozo mbaya wa kibinadamu unaoweza kutokea na kusema; 

"Tunakadiria kuwa tayari mamia kwa maelfu ya watu wa kanda hiyo wameshaathirika, iwe moja kwa moja au vinginevyo. Raia wanakufa au wanakumbwa na majeraha yanayobadili maisha. Nyumba, maeneo ya biashara na mitaa ambayo kabla ilikuwa na shughuli nyingi inageuka magofu"

Makabiliano yanayaoendelea kila siku kati ya majeshi ya pande hizo mbili yameuweka rehani mkataba wa kusitisha mapigano uliotiwa saini Jumapili iliyopita baada ya saa 11 za mazungumzo mjini Moscow.

Pompeo atoa wito wa kuheshimiwa kwa usitishaji mapigano 

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani Mike Pompeo ametoa wito kwa kila upande kuheshimu wa makubaliano hayo, wakati kundi la mataifa yenye nguvu liitwalo OSCE Minsk likionya juu ya athari mbaya za mzozo huo.

Picha: Russian Foreign Ministry/AP Photo/picture-alliance

Kundi hilo la mataifa ya Urusi, Ufaransa na Marekani ambalo kwa miaka kadhaa linaongoza juhudi za kumaliza mzozo wa Karabakh limesema hatua za haraka zinahitajika kunusuru maafa yanayoendelea kutokea.

Hata hivyo kundi hilo limekuwa likitofautiana pakubwa kimtazamo na miongo mitatu ya kujaribu njia za kidiploamisa zimeambulia patupu.

Jimbo la Azerbaijan la Nagorno Karabakh, lenye wakaazi wengi wenye asili ya Armenia, limekuwa chini ya udhibiti wa Armenia tangu vita vya miaka ya 1990 vilivyozuka baada ya kuanguka kwa uliokuwa muungano wa kisovieti.

Mapigano ya hivi sasa ndiyo makali zaidi tangu mwaka 1994 wakati makubaliano ya kusitisha mapigano yalipomaliza vita baada ya enzi ya himaya ya kisovieti.