Armenia yatoa wito wa kuwepo Ujumbe wa UN Nagorno Karabakh
24 Septemba 2023Wito huo umetolewa baada ya Azerbaijan kutangaza kuchukua udhibiti wa eneo hilo linalozozaniwa na kuahidi kuheshimu haki za jamii ya walio wachache.
Tangu operesheni kubwa ya kijeshi ya Azerbaijan katika eneo hilo la milimani, wanadiplomasia wakuu wa nchi hizo mbili walishindana kwa hoja mbele ya Baraza kuu la Umoja wa Mataifa huku mataifa ya Magharibi yakidhihirisha wasiwasi wao.
Wito wa Armenia umetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje Ararat Mirzoyan ambaye ameishutumu Jumuiya ya kimataifa kwa kutochukua hatua kufuatia operesheni ya kijeshi ya Azerbaijan ya kuchukua udhibiti wa mkoa unaozozaniwa wa Nagorno-Karabakh.
Akizungumza kwenye Mjadala Mkuu wa Umoja wa Mataifa mjini New York siku ya Jumamosi, Mirzoyan amesema jumuiya ya kimataifa na Umoja wa Mataifa zimeshindwa kuwaokoa watu.
Waziri huyo ametoa wito wa kuwepo kwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa utakaofuatilia hali jumla ya haki za binadamu pamoja na usalama katika eneo hilo.
Waziri Mkuu wa Armenia Nikol Pashinyan na Rais wa Azerbaijan Ilham Aliyev watahudhiria mkutano uliopangwa kufanyika Oktoba 5 nchini Uhispania. Mazungumzo hayo huko Grenada yatajumuisha Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Charles Michel.
Waarmenia 120,000 kuondoka Nagorno-Karabakh
Taarifa hiyo inajiri wakati utawala wa jamii ya Waarmenia imesema siku ya Jumapili kuwa watu wapatao 120,000 wa huko Nagorno-Karabakh wataondoka kwenda nchini Armenia wakiwa hawataki kuishi katika sehemu ya Azerbaijan huku wakihofia pia mauaji ya kikabila.
Waandishi wa habari wa shirika la Reuters wamesema kuwa idadi kubwa ya magari yaliyowabeba raia, tayari yamewasili katika mpaka wa Armenia wa Kornidzor.
Nagorno-Karabakh ni sehemu ya Azerbaijan lakini sehemu kubwa ya wakaazi wake ni jamii ya Waarmenia. Kwa muda mrefu udhibiti wa eneo hilo umekuwa chanzo cha mzozo kati ya mataifa hayo mawili yaliyokuwa hapo zamani katika Muungano wa Kisovieti.
Soma pia: Waasi wa Nagorno-Karabakh kuweka chini mtutu wa bunduki
Kumbukumbu za mauaji ya watu wengi katika siku za mwisho za utawala wa Ottoman (1299-1922) ambayo Waarmenia, Marekani na wanahistoria kadhaa wanayachukulia kuwa mauaji ya halaiki, bado yameacha makovu kwa raia wa Armenia ambao wanaishutumu Azerbaijan ambayo ni mshirika wa Uturuki kwa kupanga mauaji ya kikabila.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Armenia Ararat Mirzoyan amesema katika hotuba yake kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa:
" Baada ya kushindwa kuzuia mauaji ya kimbari nchini Rwanda, Umoja wa Mataifa uliweza kuunda mfumo wa kuzuia aina hiyo ya mauaji, na kutoa ahadi ya "kamwe hayatojirudia", lakini leo hii tunakaribia tena kufeli."
Wakati wanadiplomasia hao wawili walipohudhuria kikao maalum cha Baraza la Usalama siku ya Alhamisi (21.09.2023), Waziri wa Mambo ya Nje wa Azerbaijan, Jeyhun Bayramov, ameishutumu Armenia kwa upotoshaji.
Bayramov alijieleza pia kwenye Baraza Kuu na kusema kwamba Azerbaijan, ambayo raia wengi ni Waislamu, itawaheshimu Waarmenia ambao ni Wakristo na kuwajumuisha kama raia wenye haki sawa huko Nagorno Karabakh.
Bayramov ameongeza kuwa wanaendelea kuamini kwa dhati kwamba kuna fursa ya kihistoria kwa Azerbaijan na Armenia kuanzisha uhusiano wa ujirani mwema na kuishi pamoja kwa amani.
Urusi , ambayo ilituma vikosi vya walinda amani baada ya kuzuka kwa ghasia za mwaka 2020, ilikuwa ikisimamia siku ya Jumamosi, zoezi la upokonyaji silaha kwa wapiganaji wa jamii ya Armenia. Ikiwa zoezi hilo litakamilika, linaweza kumaliza mzozo wa mara kwa mara tangu kusambarataika kwa Muungano wa Sovieti.
Marekani yatoa wito wa sheria za kimataifa kuheshimiwa
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken, ambaye alijaribu kuongoza duru tatu za mazungumzo ya kuutafutia suluhu ya kidiplomasia mzozo huo, amedhihirisha "wasiwasi mkubwa".
Akifanya mazungumzo kwa njia ya simu na Waziri Mkuu wa Armenia Nikol Pashinyan, Blinken amemueleza kuwa Marekani inaishinikiza Azerbaijan "kuwalinda raia na kutekeleza wajibu wake wa kuheshimu haki za binadamu na uhuru wa kimsingi wa wakaazi wa Nagorno-Karabakh na kuhakikisha kuwa vikosi vyake vinatii sheria za kimataifa.
Mashambulizi ya hivi karibuni ya Azerbaijan, ambayo yalisababisha vifo vya watu 200, yamepelekea kuzuka kwa maandamano nchini Armenia dhidi ya Urusi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov, akizungumza na waandishi wa habari katika hadhara kuu ya Umoja wa Mataifa, ameyashutumu mataifa ya Magharibi kwa uingiliaji wao ili kuidhoofisha Moscow lakini pia akasema utawala wa Armenia umekuwa mara kwa mara ukichochea mzozo huo.
Lavrov amekumbushia kuwa tamko lililotiwa saini mwaka 1991 katika jiji kubwa zaidi la Kazakhstan la Almaty, ambalo wakati huo liliitwa Alma-Ata, lilibaini kwamba mipaka iliyopo ya nchi zilizo huru kwa sasa na ambazo awali zilizokuwa jamhuri za Sovieti, haiwezi kukiukwa. Tamko hilo lilieza bayana kuwa Nagorno-Karabakh ni sehemu ya Azerbaijan.