1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaArmenia

Zaidi ya watu 50,000 waondoka Nagorno-Karabakh

27 Septemba 2023

Serikali ya Armenia imesema Jumatano kuwa imewapokea wakimbizi zaidi ya 50,000 kutoka jimbo la Nagorno-Karabakh. Azerbaijan kwa upande wake imearifu kumkamata aliyekuwa kiongozi mkuu wa serikali ya jamii ya WaArmenia.

Armenien Geflüchtete Bergkarabakh Aserbaidschan
Picha: Irakli Gedenidze/REUTERS

Azerbaijan imearifu kuwa kiongozi huyo wa zamani anayefahamika kwa jina la Ruben Vardanyan, mwenye umri wa miaka 55 amekamatwa siku ya Jumatano wakati akijaribu kuvuka mpaka kuelekea nchi jirani ya Armenia, kufuatia harakati za kijeshi za Azerbaijan wiki iliyopita ili kurejesha udhibiti wa eneo hilo. Mke wa Vardanyan, Veronika Zonabend, amethibitisha taarifa ya kukamatwa mume wake ambaye sasa amerejeshwa mjini Baku.

Taarifa ya kukamatwa kwa Ruben Vardanyan, ambaye alikuwa mfanyabiashara bilionea nchini Urusi na aliyeongoza serikali isiyotambulika rasmi ya  "Artsakh"  kuanzia mwezi Novemba mwaka 2022 hadi Februari, 2023, ilitangazwa na maafisa wa ulinzi wa mpakani wa Azerbaijan, na hii ikiashiria nia ya Azerbaijan kudhihirisha udhibiti wao huko Nagorno-Karabakh baada ya mashambulizi ya kijeshi ambayo yamepelekea makumi ya maelfu ya jamii za Waarmenia kuondoka nchini humo.

Jamii ya WaArmania wakiondoka katika Jimbo linalozozaniwa la Nagorno-Karabakh nchini Azerbaijan wakielekea Armenia:26.09.2023Picha: Stepan Poghosyan/Photolure photo/AP Photo/picture alliance

Tangu kuanza kwa operejeshi kubwa ya kijeshi ya Azerbaijan, Armenia imetangaza siku ya Jumatano kuwa tayari imewapokea wakimbizi wapatao 50,243 wa Nagorno-Karabakh, ikiwa ni zaidi ya theluthi moja ya wakazi wa jamii hiyo ya WaArmenia wanaotaka kujitenga. Baadaye leo, Yerevan imebaini kuwa karibu nusu ya wakaazi wa Nagorno-Karabakh wanaokadiriwa kufikia 120,000 wameondoka eneo hilo.     

Soma pia: Azerbaijan yasema zaidi ya wanajeshi wake 100 wamekufa kwenye operesheni ya kuwania Nagorno Karabakh

Siku ya Jumapili, Azerbaijan ilifungua barabara pekee inayotoka eneo hilo kuelekea Armenia, ikiwa ni siku nne baada ya waasi kukubali kuweka chini silaha zao, kwa kuzingatia makubaliano ya kusitisha mapigano ambayo yanaliweka eneo linalozozaniwa chini ya udhibiti kamili wa Baku.

Jaribio la serikali ya Yerevan la kuendelea kuwashughulikia maelfu ya wakimbizi kutoka Nagorno-Karabakh wasio na makazi wala chakula, limezusha mgogoro wa kisiasa na kumuathiri mno Waziri mkuu wa Armenia Nikol Pashinyan ambapo raia wameishinikiza serikali kuwapokea wakimbizi zaidi.

Kumbukumbu ya wahanga wa vita vya mwaka 2020

Wanajeshi wa Azerbaijan wakipeperusha bendera ya taifa lao.Picha: Emrah Gurel/AP Photo/picture alliance

Leo hii pia Azerbaijan imeadhimisha kumbukumbu ya wahanga wa vita vya mwaka 2020 huko Nagorno-Karabakh. Ndugu na jamaa wa wanajeshi waliouawa katika mzozo huo walitembelea makaburi ya Baku na kutoa heshima kwa wapendwa wao. Dakika moja ya ukimya ulishuhudiwa kwenye kituo cha ukaguzi cha Lachin kwa heshima ya wale waliokufa.

Mshiriki wa vita vya pili vya Nagorno-Karabakh Salamullah Yolchuyev amesema:

"Nina furaha na huzuni kwa wakati mmoja. Nina huzuni kwa sababu tumewapoteza wapendwa wetu waliojitolea. Nina furaha kwa sababu ardhi yetu haikaliwi tena. Tumeona manufaa ya vita."

Soma pia: Mripuko wa kituo cha mafuta wauwa 20 Nagorno-Karabakh

Maafisa wa Armenia wanaendelea pia kuwatafuta zaidi ya watu 100 walioripotiwa kutoweka katika mlipuko wa bohari ya mafuta uliogharimu maisha ya watu wasiopungua 68. Moto huo ulizuka wakati wakimbizi kutoka eneo hilo walipokuwa wakijaza mafuta kwa ajili ya kuianza safari ndefu kwenye barabara yenye milima kuelekea Armenia.

(Vyanzo: DPAE, AFPE, RTRE)