1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Armstrong: Kuiacha "Livestrong" pigo kubwa

19 Januari 2013

Aliyekuwa bingwa mara saba wa mbio za baskeli maarufu kama ''Tour de France'' Mmarekani Lance Armstrong, amesema kuwa kujiuzulu kama kiongozi wa wakfu wa Livestrong lilikuwa pigo kubwa zaidi kwake.

Monday, Jan. 14, 2013 photo provided by Harpo Studios Inc., cyclist Lance Armstrong listens to a question from Oprah Winfrey during taping for the show "Oprah and Lance Armstrong: The Worldwide Exclusive" in Austin, Texas. The two-part episode of "Oprah's Next Chapter" will air nationally Thursday and Friday, Jan. 17-18, 2013
Lance Armstrong verzweifeltPicha: dapd

Armstrong amesema kwamba kujiuzulu kama kiongozi wa wakfu wa Livestrong aliouanzisha kupambana na ugonjwa wa saratani, lilikuwa tukio chungu zaidi kwake tangu kuanza kwa kashfa ya matumizi ya madawa ya kumuongezea nguvu. Aliumia zaidi na hatua hiyo kuliko hata hatua za kupokonywa mataji ya Tour de france, kupigwa marufuku kushiriki mashindano.

Armstrong ameyasema hayo katika sehemu ya pili ya mahojiano aliiyofanyiwa na mwendeshaji nguli wa vipindi vya kijamii vya televisheni nchini Marekani, Oprah Winfrey.

Armstrong amesema uamuzi wa kuachia ngazi katika wakfu huo ulikuwa mgumu kwake kuliko hata kitendo cha kuwekwa hadharani kwa visa vyake vya kutumia madawa ya kuongeza nguvu, kuzuiwa kushiriki mashindano ya mbio za baiskeli milele pamoja na kupokonywa mataji yake yote saba ya Tour de France.

Lance Armstrong akiwa katika mashindano ya Tour de FrancePicha: Getty Images/AFP

Ameongeza kuwa uchungu ulikithiri baada ya kuambiwa aachie nafasi yake ya mwenyekiti na mambo yakawa mabaya zaidi wiki mbili baadae alipoamriwa kuachana kabisa na wakfu huo na asihusike nayo kwa lolote.

Hata hivyo mwanamichezo huyo amesema kuwa hatua hiyo ni muhimu kwa maendeleo ya wakfu wa Livestrong. Amstrong alikiri katika sehemu ya kwanza ya mahojiano yake na Oprah kuwa alitumia dawa za kuimarisha misuli katika mashindano ya Tour de France ambapo alinyakua mataji saba.

Ndio, napenda kerejea mashindanoni

Alipoulizwa kama angependa kushiriki tena mashindano ya mbio hizo hata baada ya kupigwa marufuku milele, Armstrong alijibu "ndio, bila shaka, mimi ni mshindani''. ''Michezo ni kitu ambacho nimekuwa nikifanya katika maisha yangu yote. Napenda kufunza mbio za baiskeli. Napenda kushindana katika mchezo huo" aliongeza Armstrong.

Lakini hamu ya mwanamichezo huyo kurejea ulingoni ipo kwa mashindano mengine na sio Tour de France. "Nastahiki kupewa adhabu. Sina uhakika kama nastahiki kupewa adhabu ya kifo", alisema.

Lance Armstrong akiwa katika mahojiano na Oprah WinfreyPicha: dapd

Tayari Kampuni ya kuandaa filamu nchini Marekani ya JJ Abraham pamoja na ile ya Bad Rot zimepanga kutengeneza filamu kuhusu tukio hilo. Kampuni hizo tayari zimenunua haki za kitabu cha mwandishi wa gazeti la New York Times Juliet Macur ambaye amekuwa akiandika habari kuhusu Armstrong katika mataji yake saba aliyopata.

Kitabu hicho kilichopewa jina la ''Cycles of Lies: The fall of Lance Armstrong'' kinatarajiwa kuingia sokoni mwezi June mwaka huu.

Mwandishi: Stumai George/Reuters/AFP/AP

Mhariri: Daniel Gakuba

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW