1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MichezoUingereza

Arsenal watetereka tena, Man City watabasamu

17 Aprili 2023

Matumaini ya Arsenal kulibeba taji la ligi kuu ya England baada ya takriban miongo miwili yanaonekana kuanza kufifia sasa baada ya kuzuiwa kwa mara nyengine sare ya mabao mawili na watani wao wa London West Ham United.

Fußball | Champions League | Manchester City - RB Leipzig | Erling Braut Haaland
Picha: Dave Thompson/AP Photo/picture alliance

Mabao ya Gabriel Jesus na Martin Odegaard yalijibiwa na Said Benrahma na Jared Bown baada ya Bukayo Saka kukosa mkwaju wa penalti ambao ungewahakikishia pointi tatu Arsenal katika mechi hiyo.

Kwa sasa Arsenal wana pointi 74 pointi 4 mbele ya City ila the gunners wamecheza mechi moja zaidi na Jumatano ya wiki ijayo Manchester City watakuwa wanawakaribisha Arsenal uwanjani Etihad mjini Manchester.

Huyu hapa kocha wa Arsenal Mikel Arteta akizungumzia mkwaju wa penalti alioukosa nyota wake Bukayo saka katika mechi yao na West Ham.

Kocha wa Manchester City Pep GuardiolaPicha: Carl Recine/Reuters

"Kama umejiandaa kuchukua jukumu la kupiga penalti ni lazima ujue kwamba kuna uwezekano kamili wa kukosa kufunga. Utafikia wakati utakosa penalti na hustahili kuvunjika moyo. Bukayo amepitia kipindi hicho na atakipitia tena," alisema Arteta.

Man City wanatisha kila wanapoingia uwanjani

Huku Arsenal wakipoteza pointi City wao wanazinyakua kila wanapoingia uwanjani. Hapo Jumamosi walicheza na Leicester na wakavuna ushindi wa 3-0 mfungaji wao bora Erling Haaland akiendelea kuvunja rekodi za ufungaji kwani magoli mawili aliyoyafunga kwenye mechi hiyo yalimpelekea kuifikia rekodi ya Mohammed Salah ya mabao 32 katika msimu mmoja wa ligi.

Huku ikiwa zimesalia mechi nane, Haaland ana uwezo wa kuivunja rekodi ya Andy Cole na Alan Shearer ya kufunga mabao 34 katika msimu mmoja wa ligi, iwapo atatikisa wavu katika mechi hizo zijazo.

Kocha wake Pep Guardiola lakini anamtaka ajitume zaidi.

"Anaweza kuzivunja rekodi zote, uwezekano upo na inamaanisha kufunga magoli mengi na hilo litatusaidia. Ila nafikiri anachotaka ni kushinda mataji na bado tunaweza. Ila hatua hii ni hatua nzuri kwa kuwa bado kumesalia mechi nane au tisa na anakaribia kuzivunja rekodi zote," alisema Guardiola.

Chanzo:Reuters/AP

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW