Arsenal yasaka kombe la FA
22 Mei 2017Arsenal London iko katika nafasi nzuri ya kuibuka washindi wa kombe la FA nchini Uingereza kwa kuiangusha Chelsea katika fainali kwa kuwa wanahamasa ya juu kumaliza msimu huu kwa mafanikio baada ya kushindwa kufuzu kucheza katika Champions League, amesema kocha wa mabingwa wa ligi ya Uingereza , Premier League Chelsea Antonio Conte.
Chelsea walianza sherehe za ubingwa baada ya kuishinda Sunderland kwa mabao 5-1 siku ya Jumapili na wanaweza kushinda vikombe viwili vya nyumbani kwa kuishinda Arsenal, ambao wameshindwa kuingia katika timu nne bora za ligi hiyo licha ya kushinda kwa mabao 3-1 dhidi ya Everton jana Jumapili.
Conte anaweza kuwa kocha wa pili kushinda mataji mawili katika msimu wake wa kwanza baada ya Mtaliani mwenzake Carlo Anceloti kufanya hivyo katika msimu wa 2009-10. Real madrid nao wametawazwa mabingwa wa La Liga nchini Uhispania , na kuivua taji hilo Barcelona kwa mara ya kwanza katika muda wa miaka 5, na hili ni taji lao la 33. Nao Juventus Turin imefanikiwa kwa mara ya 6 mfululizo kuwa mabingwa wa Italia. AS Monaco wametawazwa mabingwa wa ligi ya Ufaransa Leage 1 kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2000.
Manchester United na Ajax Amsterdam zinakutana katika fainali ya kombe la Ulaya siku ya Jumatano katika pambano la vigogo wa zamani wa bara hili. Ajax na Manchester United zina nafasi ya kulinyakua taji la ligi ya Ulaya siku ya Jumatano wakati timu zote zina lengo la kupiga hatua nyingine kurejea katika medani ya vigogo vya soka la Ulaya. Kwa Ajax mabingwa mara nne wa Ulaya , mchezo huo wa fainali mjini Stockholm ni wa kwanza katika bara la Ulaya tangu mwaka 1996, wakati walipopoteza ubingwa wa Champions league kwa mikwaju ya penalti.
United itakuwa katika fainali ya Ulaya tangu mwaka 2011 ambapo ilipoteza fainali ya Champions League dhidi ya Barcelona , na kwa hakika inanafasi nzuri kuliko wapinzani wao.
Mwandishi: Sekione Kitojo
Mhariri: Mohammed Khelef