1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Arteta: Martinelli alikuwa hajapona jeraha dhidi ya City

9 Oktoba 2023

Kocha wa Arsenal Mikel Arteta anasema winga wa klabu hiyo Gabriel Martinelli alicheza mechi ya Jumapili dhidi ya Manchester City na kufunga goli la ushindi licha ya kuwa alikuwa hajapona vyema jeraha alilokuwa nalo.

Ligi Kuu ya England | Mikel Arteta
Kocha wa Arsenal Mikel ArtetaPicha: Kirsty Wigglesworth/AP Photo/picture alliance

Martinelli aliingia uwanjani katika kipindi cha pili alipoichukua nafasi ya Leandro Trossard na kuelekea mwishoni mwa mechi akafunga goli la pekee lililowahakikishia pointi tatu Arsenal na kuwapelekea kileleni mwa ligi ya nchi hiyo hiyo kuelekea mapumziko ya mechi za kimataifa.

"Kwa wiki chache sasa amekuwa akisema atakuwepo dhidi ya City na kila mmoja akawa anamwambia, Gabby itakuwa mapema sana kwako. Na jana akasema, bosi nilikwambia nitakuwa tayari kwa mechi hii. Na baada ya Trossard kuumia baada ya nusu saa, nilipogeuka nikaona yuko tayari. Kwa hiyo ni kijana ambaye hali yake ya kisaikolojia ni zaidi ya umri wake na ni furaha kuwa naye kwa kuwa leo amesaidia sana sisi kushinda mechi," alisema Arteta.

Kocha wa Manchester City Pep Guardiola yeye anasema matokeo ya Jumapili hayajampa kiwewe kwa kuwa msimu bado ni mrefu licha ya kuwa hiyo ya jana ilikuwa mechi ya pili mfululizo kwa City kupoteza katika ligi baada ya kufungwa na Wolverhampton Wanderers 2-1 wiki mbili zilizopita.

Kocha wa Man City Pep Guardiola na mshambuliaji wake Erling HaalandPicha: SCOTT HEPPELL/REUTERS

"Hatujazoea kushindwa ila ni kandanda, inatokea. Takwimu zinaonyesha hatuna ulazima wa kushinda ligi, hakuna timu ambayo imeshinda mataji 4 mfululizo. Ila bado ni mwezi Oktoba, wakati mwengine ni vizuri kuwa nyuma. Si mara ya kwanza tumekuwa nyuma ya wanaoongoza, msimu uliopita tulikuwa nyuma sana. Ila msimu ni mrefu," alisema Guardiola.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW