Artur Mas ashindwa Catalonia
26 Novemba 2012Chama cha waziri mkuu huyo Artur Mas cha CiU kimepata viti 50 kutoka 62 vya awali kati ya jumla ya viti 135. Licha ya kushindwa huko, bunge jipya la jimbo hilo litadhibitiwa na makundi yanayopendelea kujitenga.
Hajutii uamuzi wake
Mas na chama chake wamepoteza uungwaji mkono. Alikuwa akitarajia kupata wingi zaidi wa viti katika bunge hilo jipya. Badala yake chama chake kilipoteza viti 12 na atahitaji kutafuta mshirika ili kuunda serikali ya mseto. Kampeni yake iliendeshwa kwa misingi ya kupigania uhuru wa jimbo la Catalonia, na aliitisha uchaguzi huo miaka miwili kabla ya muda wake. Lakini ujumbe wake haukuwafikia wapiga kura kama ilivyotarajiwa.
"Baadhi watasema kwamba hakukuwa na umuhimu wa kuendesha uchaguzi wa mapema, hasa kwa kuzingatia kuwa aliyeitisha uchaguzi huo ameshindwa katika kura, lakini bila shaka sijutii uamuzi wangu huo," aliwambia wafuasi wake baada ya kutangazwa kwa matokeo.
Madai ya uhuru bado yako pale pale
Licha ya kushindwa kwa chama cha CiU, bado kuna uungaji mkono mkubwa wa suala la uhuru wa Catalonia. Chama chenye msimamo mkali cha mrengo wa kushoto cha ERC kiliendesha kampeni kubwa kikiunga mkono uhuru, na kiliongeza viti vyake mara mbili kutoka kumi hadi 21, na hilo linavihakikishia vyama vinavyotaka kujitenga wingi wa wabunge. Mas anatarajiwa kuungana na chama cha ERC, ambacho kimekosoa vikali mipango yake ya kupunguza matumizi katika sekta za afya na elimu.
Mas anataka kuendesha kura ya maoni katika miaka minne ijayo lakini serikali kuu mjini Madrid imeapa kuzuia mipango yake katika mahakama ya katiba. Wakosoaji wake wanasema alichochea kampeni ya uhuru ili kuwapotezea lengo raia, ambao wanachukizwa na mipango yake ya kupunguza matumizi katika sekta za kijamii. Kiongozi wa chama cha Catalan People's Party Alicia Sanchez-Camacho alimtaka Mas kukubali kushindwa na kuachana na msimamo wake wa kujitenga.
Misukosuko ya kiuchumi Catalonia
Jimbo la Catalonia, lenye ukubwa sawa na Ubelgji lilikuwa linabeba uchumi wa Uhispania, lakini hivi sasa limeathiriwa na mgogoro wa kiuchumi, na serikali yake ililaazimika kuomba msaada kutoka serikali kuu. Mas anasema Catalonia ingeweza kukabiliana na matatizo yake ya kiuchumi kama isingelaazimishwa kupeleka sehemu ya mapato yake kwenye mikoa maskini zaidi ya Uhispania.
Waziri mkuu Rajoy anakabiliwa na vuguvugu jingine la uhuru katika jimbo la Basque, ambako kujisalimisha kwa kundi lenye silaha la ETA mwaka 2011 kuliviongezea nguvu vyama vinavyopigania uhuru wa jimbo hilo kwa njia ya amani. Kabla ya kufanyika kwa kura hiyo, serikali kuu iliiomba mahakama ichunguze madai kuwa Artur alihusika katika sakata la rushwa katika ukumbi wa maonyesho mjini Barcelona. Waziri mkuu huyo alipinga madai hayo na kusema kuwa ni njama za kisiasa zinazolenga kuchafua vuguvugu la uhuru.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/dpae
Mhariri: Daniel Gakuba