1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Asasi za kiraia Kenya kupokea taarifa wakati wa uchaguzi

2 Agosti 2022

Ikiwa imesalia wiki moja tu kuelekea katika uchaguzi mkuu nchini Kenya, wanaharakati kutoka asasi za kiraia wamezindua ukumbi maalum wa kupokea taarifa kutoka kwa raia na makundi ya waangalizi wakati wa uchaguzi mkuu.

Kenia | Wahlkampf
Picha: James Wakibia/Zuma/picture alliance

Katika hafla iliyoandaliwa na mashirika mbalimbali, na kuhudhuriwa na wawakilishi kutoka asasi za kiraia, wasemaji akiwemo Angela Lungati mkurugenzi mtendaji wa kampuni maarufu ya teknolojia nchini Kenya iitwayo Ushahidi, wameelezea hofu yao kuhusu ongezeko la maneno mazito yanayotumiwa katika mitandao ya kijamii, hali ambayo inaweza kuchochea machafuko.

Angela Lungati ni mkurugenzi mtendaji wa kampuni maarufu ya teknolojia nchini Kenya iitwayo Ushahidi. 

Kulingana na wadau wa mpango huo, lengo la ukumbi huo unaofahamika kama ‘Uchaguzi Platform' ni kupokea taarifa na ripoti kuhusu visa vya uhalifu na matukio mengine yanayoambatana na zoezi la uchaguzi kutoka kwa raia na makundi ya waangalizi.

''Mchakato huu ni jitihada za pamoja kutoka mashirika ya kijamii na asasi za kiraia za kuendeleza utoaji wa habari muhimu kwa umma na pia kuwezesha hatua za haraka kuchukuliwa kisheria endapo kutakuwepo na visa vyovyote vya uhalifu au machafuko wakati wa zoezi la uchaguzi,'' alifafanua Ann Ireri mwenyekiti wa kundi la waangalizi wa uchaguzi la ELOG.

Tayari makundi ya waangalizi wa uchaguzi kutoka nje na ndani ya nchi wameanza kuwatuma mawakala wake katika kila pembe ya nchi kwa maandalizi ya kupiga darubini matukio ya uchaguzi mkuu ifikapo Jumanne.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW