1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ASEAN na washirika wengine wasaini mkataba wa kibiashara

16 Novemba 2020

Mataifa 10 ya Asia na nchi nyingine tano za Asia Pasifiki zimesaini makubaliano ya biashara huriai. Mkataba huo unatarajiwa kusaidia ukuaji wa uchumi katika ukanda huo ulioathirika vibaya na janga la virusi vya corona.

Vietnam Hanoi | Abschluss virtueller ASEAN-Gipfel | Freihandelsabkommen
Picha: Kham/REUTERS

Makubaliano hayo yaliyosainiwa Jumapili pembezoni mwa mkutano wa kilele uliofanyika kwa njia ya video mjini Hanoi, Vietnam, yamefikiwa baada ya miaka minane ya mazungumzo yaliyogubikwa na changamoto nyingi. Mwenyeji wa mkutano huo, waziri Mkuu wa Vietnam, Nguyen Xuan Phuc amesema makubaliano hayo ya ushirikiano wa kiuchumi wa kikanda, RCEP, ni muhimu sio tu kwa Jumuia ya Ushirikiano wa Mataifa ya Kusini Mashariki mwa Asia, ASEAN, lakini pia kwa uchumi wa dunia.

''Makubaliano haya yanaweza kuurekebisha mfumo wa ugavi ulimwenguni na kusambaza kwa ufanisi biashara na uwekezaji wa nchi za ASEAN na washirika wake kadhaa. Yanaweza pia kupunguza athari kubwa za kiuchumi kwenye baadhi ya nchi katika muktadha wa kuzuia na kulidhibiti janga la virusi vya corona, pamoja na kukuza uzalishaji, huku yakitatua matatizo ya ajira kwa watu,'' alifafanua Nguyen.

Soma zaidi: Viongozi wa ASEAN kuafikiana juu ya mkataba wa RCEP

Ushirikiano huo wa RCEP unawajumuisha watu bilioni 2.2 na asilimia 29 ya pato la uchumi duniani. Nchi zilizosaini makubaliano hayo katika mkutano wa kilele wa 37 wa mataifa ya ASEAN ni pamoja na Vietnam, Thailand, Ufilipino, Laos, Cambodia, Myanmar, Malaysia, Indonesia, Brunei na Singapore. Nchi nyingine ni pamoja na Australia, China, Japan, New Zealand, na Korea Kusini.

​​​​Waziri Mkuu wa China, Li Keqiang ameusifu ''mkataba huo wa kihistoria''Picha: Nhac NGUYEN/AFP

Waziri Mkuu Nguyen amesema tangu mwanzoni mwa 2020, janga la virusi vya corona limeziingiza zaidi ya nchi 200 katika changamoto kubwa za kijamii, kiuchumi na kisiasa na kupunguza kiwango cha biashara na uwekezaji ulimweguni. Amebainisha kuwa wameshuhudia juhudi mbalimbali zikifanyika katika kuyatatua masuala yaliyopo kwa njia ya mazungumzo.

Yaliyomo ndani ya makubaliano

Mkataba huo utapunguza ushuru, utafungua sekta ya huduma na kuweka sheria za kawaida za biashara ndani ya kanda hiyo. Pia unajumuisha huduma za kibiashara, uwekezaji, biashara kupitia mtandao wa intaneti, mawasiliano ya simu na hakimiliki. Hata hivyo, utunzaji wa mazingira na haki za ajira, sio sehemu ya mkataba huo.

Makubaliano hayo yanayoungwa mkono na China yanaonekana kama mbadala wa Mkataba wa Biashara Huria katika Ukanda wa Bahari ya Pasifiki, TTP, ambao Marekani ilijiondoa.

Nchi ambayo haikuonekana katika mkutano huo wa RCEP ni India ambayo ilijiondoa katika mazungumzo ya 2019, kwa madai kwamba ina wasiwasi kuhusu kufungua sekta zake za kilimo na viwanda kwa washindani wake wa kigeni. Hata hivyo, viongozi wa ASEAN wamesema bado wana nia ya kushirikiana kibiashara na India na kwamba mlango bado uko wazi kwa India kujiunga tena na umoja huo.

(AFP, DPA, AP)

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW