ASEAN yakataa kuidhinisha uchaguzi wa kijeshi Myanmar
20 Januari 2026
Jumuiya ya Umoja wa Mataifa ya Kusini-Mashariki mwa Asia (ASEAN) haitaidhinisha uchaguzi uliofanyika nchini Myanmar inayotawaliwa na jeshi, waziri wa mambo ya nje wa Malaysia amesema. Sababu kuu ni ukosefu wa ushiriki huru, wa wazi na jumuishi katika mchakato wa uchaguzi huo.
Kauli hiyo inakuja baada ya chama kinachoungwa mkono na jeshi kuonekana kuelekea kupata wingi wa viti bungeni, kufuatia duru ya pili ya upigaji kura mapema mwezi huu. Huo ulikuwa uchaguzi wa kwanza wa kitaifa tangu jeshi lilipoiondoa serikali ya kiraia ya Aung San Suu Kyi mwezi Februari 2021, hatua iliyosababisha maandamano makubwa na hatimaye vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Makundi ya haki za binadamu na vyama vya upinzani yamesema uchaguzi huo haukuwa huru wala wa haki. Yameutaja kama jaribio la jeshi kuhalalisha utawala wake baada ya mapinduzi.
Akizungumza bungeni Jumanne, Waziri wa Mambo ya Nje wa Malaysia, Mohamad Hasan, alisema viongozi wa ASEAN waliamua katika mkutano wao wa kilele mwezi Oktoba kutotuma waangalizi wa uchaguzi nchini Myanmar. Alisema hali haikuruhusu kufanyika kwa uchaguzi wa kuaminika, ingawa baadhi ya nchi wanachama waliamua kutuma waangalizi wao binafsi.
Wizara ya Habari ya Myanmar ilisema mwezi uliopita kuwa baadhi ya wanachama wa ASEAN, zikiwemo Cambodia na Vietnam, walikuwa miongoni mwa nchi zilizotuma waangalizi. Hata hivyo, Malaysia imesisitiza kuwa hilo halikuwa uamuzi wa pamoja wa jumuiya hiyo.
ASEAN yasisitiza uchaguzi huru, wa haki na shirikishi
Mohamad Hasan alisema ASEAN imeweka wazi kuwa uchaguzi wowote lazima ufanyike kwa ushiriki kamili na huru wa wadau wote wa kisiasa. Alionya dhidi ya chaguzi zinazofanyika kwa awamu au chini ya masharti yanayowazuia wagombea fulani.
“Hatutumi waangalizi, na kwa mantiki hiyo, hatuthibitishi wala kuidhinisha uchaguzi huo,” alisema. Kauli yake imechukuliwa kama tamko la kwanza la wazi kutoka kwa jumuiya hiyo ya nchi 11 kwamba haitatambua matokeo ya uchaguzi wa Myanmar.
ASEAN imekuwa ikiishinikiza serikali ya kijeshi ya Myanmar kutekeleza mpango wa amani iliyouafiki, unaojumuisha kusitisha vurugu, kuruhusu misaada ya kibinadamu na kuanzisha mazungumzo jumuishi kati ya pande zote. Hata hivyo, utekelezaji wake umekwama.
Jumuiya hiyo ilisimamisha viongozi wa kijeshi wa Myanmar kushiriki mikutano ya kilele ya ASEAN. Pamoja na hilo, mgawanyiko ndani ya ASEAN umeathiri hatua kali zaidi, huku baadhi ya nchi zikitetea ushirikiano wa kidiplomasia na nyingine zikishinikiza shinikizo kubwa zaidi kwa majenerali wa Myanmar.
Matokeo ya mwisho ya viti vyote katika mabunge ya kitaifa na ya kikanda yanatarajiwa kutangazwa mwezi huu. Hata hivyo, bila uungwaji mkono wa ASEAN, mustakabali wa kisiasa wa Myanmar unaendelea kuwa na sintofahamu kubwa.