Ashton akutana na Mursi
30 Julai 2013Hayo yameelezwa leo(30.07.2013) na Umoja wa Ulaya, ikiwa ni mkutano wa kwanza wa kiongozi huyo anayeelemea zaidi itikadi za dini ya Kiislamu na kiongozi kutoka nje ya nchi hiyo tangu pale jeshi la Misri lilipomuondoa madarakani karibu mwezi mmoja uliopita.
Mkuu wa sera za mambo ya kigeni wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton alikutana na Morsi jana jioni(29.07.2013) , kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa katika ukurasa wa Twitter na msemaji wa Ashton, Maja Kocijancic. Hakusema hata hivyo mkutano huo ulifanyika wapi, na hakutoa maelezo ya majadiliano hayo.
Mursi hajulikani aliko
Tangu mapinduzi ya Julai 3, ambayo yalifuatia maandamano makubwa ya mamilioni ya Wamisri wakitaka kuondolewa madarakani kwa Mursi, rais huyo wa zamani amekuwa akishikiliwa mahali pasipojulikana na jeshi bila mawasiliano na watu kutoka nje. Kundi la wanaharakati wa haki za binadamu nchini Misri lilichukuliwa na wanajeshi hadi mahali ambapo Mursi anashikiliwa na jeshi wiki hii lakini alikataa kuonana nao.
Waendesha mashitaka siku ya Ijumaa wamesema Mursi anakabiliwa na mashtaka ya kushirikiana na kundi la wapiganaji wa Kipalestina wa Hamas na kutoroka kutoka jela wakati vuguvugu wa maandamano ya umma mwaka 2011 na kuuangusha utawala wa kimabavu wa Hosni Mubarak.
Ashton yuko nchini Misri katika ziara yake ya pili mwezi huu kutafuta njia za kuitoa Misri katika umwagaji damu pamoja na mzozo wenye utata, akitafuta maridhiano katika mazungumzo na serikali inayoungwa mkono na wanajeshi pamoja na washirika wa rais aliyeondolewa madarakani.
Ashutumu mauaji
Kabla ya ziara yake , Ashton alishutumu ghasia zilizotokea mwishoni mwa juma ambapo watu 83 waliuwawa wakati wa maandamano na alitoa wito wa kufanyika hatua za kisiasa ambazo zitajumuisha makundi yote, ikiwa ni pamoja na kundi la Udugu wa Kiislamu la Mursi.
Lakini hakuna dalili kuwa kila upande wa mzozo huo uko tayari kukubaliana na miito yake. Kundi la Udugu wa Kiislamu limekataa wito wa kufanyakazi pamoja na viongozi wapya na kuitisha maandamano mapya leo. Serikali nayo haikutoa ishara ya kuleta maridhiano.
Ziara ya Ashton na mazungumzo ya simu kati yake na waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry pamoja na viongozi wa Misri yanaonesha hali ya jumuiya ya kimataifa kuona umuhimu wa kuchukua hatua za haraka, ambapo viongozi wake wanahimiza zaidi hatua za kisiasa ambazo zitajumuisha makundi yote hatua ambazo zitamaliza ghasia.
Kundi la Udugu wa Kiislamu na washirika wake linadai kuwa Mursi ni lazima arejeshwe madarakani, lakini serikali inayoungwa mkono na jeshi inataka kuendelea mbele na mpango wake wa mpito ambao utaelekeza katika uchaguzi wa bunge na rais mapema mwakani.
Wakati huo huo jeshi la Misri limesema limechunguza ripoti kuwa kulikuwa na mripuko katika eneo la mfereji wa Suez lakini ripoti hizo si za kweli na halikupata ushahidi wa tukio hilo.
Mwandishi : Sekione Kitojo / ape
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman