1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Asia inakumbuka Miaka 60 baada ya vita kumalizika

Lillian Urio15 Agosti 2005

Bara la Asia linakumbuka miaka 60 baada ya vita vikuu vya pili vya dunia kumalizika. Naye Waziri Mkuu wa Japan, Junichori Koizumi, ameomba msamaha kwa matendo yaliofanywa na nchi yake wakati wa vita hivyo.

Waziri Mkuu Koizumi ameomba msamaha, kwa mara nyingine tena mwaka huu, kwa matendo maovu yaliofanywa na nchi yake wakati wa vita vya pili vya dunia.

Wakati huo huo, mawaziri wake wawili wanategemea kuhudhuria sehemu takatifu kwa Wajapani, Yasukuni, iliyopo mjini Tokyo kwa ajili ya mashujaa wa kivita.

Lakini pamoja na kwamba watu milioni mbili na nusu waliokufa wakati wa vita wanakumbukwa, mataifa mengine ya bara hilo wanalalamika kwamba sehemu hiyo pia inawatukuza wahalifu wa kivita.

Kwa maoni ya nchi za jirani za Uchina na Korea Kaskazini na Kusini wahalifu wa kivita wanaotukuzwa hapo Yasukuni hawafai kukumbukwa kwa heshima na viongozi wa ngazi za juu wa seriklai ya Japan.

Pamoja na kuomba msamaha kwa mara nyingine tena, Waziri Mkuu Koizumi anategemewa kutotembelea sehemu hiyo ya kuwakumbuku wafu wa kivita mwaka huu.

Katika ujumbe wake wa wazi kwa nchi za jirani, Waziri Mkuu huyo alisema anahuzunika sana jinsi nchi yake ilivyotawala kwa nguvu na ukatili katika nchi za jirani wakati wa vita.

Aliongeza kwamba nchi yake ilisababisha mateso makubwa kwa watu wengi duniani, hasa katika mataifa ya bara la Asia, kupitia ukoloni na uvamiaji. Na alitoa pole kwa wahanga wote wa vita hivyo nchini kwake na nje.

Mwezi Aprili mwaka huu Waziri Mkuu Koizumi aliomba msamaha kwa nchi za jirani wakati wa mkutano mkuu wa bara la Asia uliofanyika mjini Jakarta, Indonesia.

Gazeti la taifa kila siku la Uchina liliandika kwamba Waziri Mkuu Koizumi hasikilizi malalamiko yao kwa sababu anataka kuwafurahisha Wajapani wenye msimamo mkali, ambao wanaamini kinachotakiwa kufanyika ni kutotatua tatizo hilo.

Serikali ya Uchina iliamua kuongeza ulinzi njee ya nyumba ya balozi wa Japani, mjini Beijing, kwa sababu tayari maandamano yaliozua vurugu yalifanyika mwaka huu sehemu hiyo.

Lakini Kusini-Mashariki mwa bara la Asia, sehemu ambayo pia watu waliteseka chini ya utawala wa nguvu wa Japan, inaelekea hamna chuki ya hali ya juu dhidi ya nchi hiyo. Hii ni kutokana na miaka mingi ya Japan kutoa misaada na kuwekeza katika eneo hilo na kupelekea uchumi wa nchi hizo kukua.

Nchini Philippines watu laki moja walikufa katika mapigano ya kipindi cha mwezi moja yalioharibu kabisa mji mkuu wa Manila mwaka 1945. Kumbukumbu pekee iliyofanyika ni ya wagongwe wa Kiuchina na Kifilipino.

Kuna wanaodhani kuwa taifa hilo kutokuwa na chuki dhidi ya Japan ni kwa sababau limesahahu yaliotokea. Wengine wanasema labda ni kwa sababu ukoloni mbaya wa Kijapani ulikuwa unafuata ule wa Hispania na Marekani

Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea Kusini imesema matamko tofauti ya wanasiasa wa Japan yanawapa wasiwasi juu ya ukweli wa maombi ya msamaha ya nchi hiyo.

Watoto, wanafunzi na watu wazima, wakichanganjika na wazee na wagongwe waliovaa suti nyeusi wamekuwa wakitembelea Yasukuni. Ulinzi wa polisi ulikuwepo kwenye eneo hilo ili kuzuia mzozo wowote usitokee kati ya makundi ya wanaounga mkono Yasukuni na wale wanaopinga.
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW