1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Asia inaweza kuwa eneo jipya kwa kundi la IS?

5 Mei 2019

Kundi linalojiita Dola la Kiislam linaweza kuwa limesambaratishwa katika eneo la Mashariki ya Kati lakini bara la Asia linatoa nafasi muafaka ya kuibuka upya kwa kundi hilo.

Syrien Angriff auf IS Stellungen in Baghouz
Picha: Getty Images/AFP/G. Cacace

Hilo linasemwa na wachambuzi wa masuala ya usalama wakipigia mfano mashambulizi ya kutisha ya mwezi uliopita nchini Sri Lanka wakati wa sikukuu ya Pasaka. 

Masuala kama umasikini, kutengwa kwa baadhi ya makundi ndani ya jamii, uhamasishaji itikadi kali kupitia mitandao ya kijamii, utawala dhaifu na udhaifu kwenye kukusanya na kubadilishana taarifa za kiintelejensia kunamaanisha eneo hilo limo kwenye hatari kubwa ya kushambuliwa na wafuasi wa itikadi kali wanaoendesha operesheni zao kwa mwavuli wa kundi la IS hata kama hawaungwi mkono moja kwa moja na kundi hilo.

Kundi la IS lilipoteza udhibiti wa eneo lake la mwisho Mashariki yakati mwishoni mwa mwezi Machi lakini wachambuzi walionya kushindwa kwao hakutofifisha itikadi yao, na ni wiki chache tu baadaye kundi hilo lilidai kuhusika na moja kati ya mashambulizi mabaya kabisa ya wanamgambo dhidi ya raia barani Asia.

Mchambuzi Scott Stewart amesema katika ripoti mpya kwa ajili ya taasisi ya kijasusi ya Marekani kuwa hali ya sasa ya kundi la dola la Kiislam haiwezi kupimwa bila kuelewa kuwa wanachofanya ni vuguvugu la itikadi linaloendelea dunia nzima na siyo suala la kundi moja.

Mashambulizi ya sikukuu ya Pasaka ni mfano hai

Picha: Getty Images/AFP/J. Samad

Mashambulizi ya mabomu kwenye makanisa na hoteli za fahari nchini Sri Lanka yalisababisha vifo vya watu zaidi ya 250 na serikali imelilaumu kundi dogo la itikadi kali  nchini humo la Thawheed Jamma'ath kuwa limehusika kwenye mkasa huo.

Picha za vidio zilizoonekana baadae zilionesha washambuliaji wakionesha utiifu na uungaji mkono kwa kundi la IS.

Idara za usalama nchini Sri Lanka zimekosolewa vikali kwa kushindwa kufanyia kazi taarifa za onyo walizopewa kutoka kwa Waislam wa nchini humo na idara ya ujasusi ya India kuhusu uwezekano wa kutokea mashambulizi.

Kadhalika serikali ya Sri Lanka imekuwa kwenye mkwamo wa kisiasa kwa miezi kati ya rais Maithripala Sirisena anayevutana na waziri wake mkuu Ranil Wikremesingha.

"Maafisa wa usalama walipewa onyo la wazi kabisa lakini lazima kuwe na kuwajibishana juu ya ni vipi na kwanini tahadhari zilizotolewa hazikufanyiwa kazi" amesema Mchambuzi Scott Stewart.

Umasikini unachangia kiasi gani?

Licha ya kwamba washambuliaji wawili wa kujitoa muhanga walikuwa ndugu kutika familia tajiri inayofanya biashara ya viungo wachambuzi wanasema hilo haliondoi ule ukweli kwamba umasikini mara zote ndiyo umekuwa chanzo cha kuongezeka kwa makundi ya wanamgambo katika sehemu nyingne barani Asia iliwemo kusini mwa Ufilipino.

Picha: Fotolia/OlegD

Sidney Jones, mkurungenzi wa Taasisi ya Uchambuzi wa Sera kwenye Mizozo amesema dini pekee haiwezi kulaumiwa kwa uasi wa muda mrefu katika kisiwa cha Mindanao nchini Ufilipino.

Badala yake ni kwa sababu watu masikini na wasio na usemi kwenye eneo hilo wanajiona ni waliotengwa kutokana na fursa za taifa zima.

Mchambuzi huyo anasema hiyo ni moja kati ya masuala yanayowafanya watu kukimbilia kuwa wafuasi wa itakadi kali kama kundi la IS linalojitokeza kuma mbadala kwa madhila yanayowakabili.

Nchini Bangladesh an Indonesia mtindo wa maisha ya Waislam wa wastani umeharibiwa na ushawishi kutoka wale wenye misimamo mikali wanaoneza ujumbe wao kupitia mtandao wa intaneti.

Mchambuzi Mubashar Hasan kutoka Chuo Kikuu cha Oslo amesema kadiri watumiaji wa mtandao wa intaneti wanavyoongezeka ndivyo ushwishi wa makundi kama IS unavyojipenyeza.

Katika wakati ambao kundi la IS limesambaratishwa mashariki ya kati nchi nyingi za Asia hivi sasa zinawasaka raia wake waliojiunga na kundi hilo na wanaojaribu kurejea nyumbani kuendeleza mapambano kwenye nchi zao.

Mtaalamu wa masuala ya ugaidi Taufik Andrie akiwa mjini Jakarta amesema akihitimisha kuwa kwa dhati kabisa mapambano ya Uislaam na wafuasi wake dhidi ya wapiganaji wa itakadi kali ni ya muda mrefu.