1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Asia na Ulaya wakubaliana kuuchunguza mfumo wa fedha duniani

Nijimbere, Gregoire25 Oktoba 2008

Viongozi wa nchi 43 kutoka Asia na Ulaya wamekamilisha mkutano wao wakikubaliana kufanya mageuzi katika mfumo wa fedha duniani.

Marais mkutanoni mjini Beijing ChinaPicha: AP

Mkutano wa kilele wa siku mbili wa viongozi wa nchi kutoka mabara ya Asia na Ulaya ulyiokuwa ukifanyika mjini Beijing China, umekamilika. Mkutano huo ulizungumzia zaidi juu ya mgogoro wa fedha duniani na juhudi za kupunguza utoaji wa gesi zinazochafua mazingira.

Viongozi wa nchi 16 za Asia na 27 za Ulaya, wamekubaliana kufanya uchunguzi wa mfumo wa fedha duniani ambao umeathiriwa na hofu za kudorora kwa uchumi na kuanguka kwa hisa. Waziri mkuu wa China, Wen Jiabao, amesema nchi zote zinahitaji kuimarisha ushirikiano. Uchina mwenyeji wa mkutano huo, imesema kunahitajika kufanywa uchunguzi wa karibu wa mfumo wa fedha duniani ili biashara inayoendeshwa kwa nyaraka iendane na fedha taslimu katika uchumi, laa sivyo hakutakuwa na mizani tena na dunia itaendelea kukumbwa na mizozo kama hiyo.

Viongozi hao wamekubaliana kushiriki katika mkutano wa kilele wa kundi la nchi 20 tajiri na zile zinazoinukia kiuchumi -G20 mjini Washington Marekani tarehe 15 mwezi ujao ambapo wanategemea kuwa zitachukuliwa hatua muhimu.

China imeahidi kuwa itashiriki.

Rais wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy na Mkuu wa Halmshauri ya Ulaya, Jose Manuel Barroso, wamesema Ufaransa na Umoja wa Ulaya, zimetimiza jukumu lao la kuzishawishi nchi za Asia kushiriki katika mkutano huo wa mwezi ujao wakiwa na matumaini kuwa utachukuwa hatua mpya za kuudhibiti kikamilifu mfumo wa fedha duniani kama makubaliano mapya ya Bretton Woods, hatua ambazo utawala wa Marekani wa rais, George W. Bush, hungependelea zichukuliwe ukidai kuwa ni kuingilia sera huru za biashara na uwekezaji.

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon ameonya akiwa mjini New York Marekani kwamba nchi masikini zaidi duniani zisisahauliwi kwa sababu nchi hizo zinahitaji misaada mikubwa hasa wakati huu mgumu.


Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW