1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafanyakazi wa nyumbani wateswa na kunyanyaswa Qatar

20 Oktoba 2020

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadam Amnesty International limetoa taarifa, wafanyakazi wa nyumbani nchini Qatar wanapitia unyanyasaji, kupigwa na kudhalilishwa na mazingira magumu ya kazi.

Libanon Beirut Migranten-Arbeiter | Protest vor Konsulat von Kenia
Picha: Anwar Amro/AFP

Baada ya kufanya mahojiano na wanawake 105, shirika hilo limebaini asilimia 85 ya wanawake walifanya kazi kwa zaidi ya saa 14 kwa siku, hawakupewa siku za mapumziko na nyaraka zao za kusafiri zilichukuliwa na waajiri wao punde tu wanapowasili nchini humo.

Miongoni mwa madhila waliyopitia wanawake hao ni pamoja na kucheleweshwa kwa mishahara au kutolipwa kabisa. Baadhi yao walikosa chakula cha kutosha au walilazimika kula mabaki. Wengine walilala chini na kunyimwa huduma za matibabu.

Vile vile kuna ambao waliripoti kuwa walikuwa wakipigwa, kutemewa mate na hata kudhulumiwa kingono.

Picha: picture-alliance/dpa/W. Kumm

"Ikiwa imethibitishwa kuwa kweli, madai yaliyotolewa na watu binafsi waliohojiwa katika ripoti ya Amnesty International ni ukiukaji wa sheria ya Qatar na lazima ishughulikiwe ipasavyo," ofisi ya mawasiliano ya serikali ya Qatar ilisema katika taarifa.

Wizara ya wafanyakazi Qatar imesema iko tayari kushirikiana na Amnesty International ili kuchunguza madai na kuhakikisha pande zote zilizo na hatia zinawajibishwa na juhudi zinaendelea kuimarisha mfumo kazi na kuhakikisha wafanyakazi wa nyumbani wanalindwa zaidi kutokana na dhuluma na unyanyasaji.

Washambulizi wa London watambulishwa

02:07

This browser does not support the video element.

Qatar ni makazi ya wahamiaji milioni 2, wengi wao wakiwa maskini kutoka Bangladesh, Nepal na India. Karibu wanawake 173,000 ni wafanyikazi wa nyumbani.

Kama mwenyeji wa Kombe la Dunia la mpira wa miguu la 2022, Qatar imekuwa chini ya uangalizi wa kimataifa.

Nchi hiyo hivi karibuni imefanya mageuzi kwa wafanyikazi wa kigeni kwa kuongeza kiwango cha mshahara, kiwango cha chini kila mwezi kuwa riyal 1,000 sawa na dola 275 za Kimarekani na kutangaza kuwa wafanyikazi wa kigeni watakuwa na uhuru wa kubadilisha sehemu ya kazi bila idhini ya mwajiri wao wa awali.

Hata hivyo shirika la Amnesty International lilisema mageuzi haya hayawezi kwa kiasi kikubwa kupunguza unyanyasaji au kuboresha hali ya wafanyikazi wa nyumbani bila kuwepo kwa hatua za ziada za kuimarisha ulinzi na kuhakikisha utekelezaji.