1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Asilimia 90 ya raia wa Tigray wanahitaji msaada wa kiutu

1 Juni 2021

Umoja wa Mataifa umetahadharisha kwamba zaidi ya asilimia 90 ya watu wa jimbo la Tigray kaskazini mwa Ethiopia wanahitaji msaada wa chakula haraka, na dola milioni 203 zinahitajika

Bildergalerie Äthiopien | Flucht aus der Region Tigray
Picha: Baz Ratner/REUTERS

Umoja wa Mataifa umesema hali hiyo imesababishwa na mgogoro wa hivi karibuni katika jimbo la Tigray.  Shirika la chakula la Umoja wa Mataifa WFP limeshtushwa kuona jinsi mgogoro huo ulivyozidisha kiwango cha njaa ambacho tayari kilikuwa cha juu katika jimbo hilo.

Msemaji wa shirika hilo Tomson Phiri ameeleza kuwa jumla wa watu milioni 5.2 yaani asilimia 91 ya wakaazi  wote wa jimbo hilo wanahitaji msaada wa chakula wa haraka. Kutokana na hali hiyo asasi hiyo imetoa mwito wa kuchangisha dola zaidi ya milioni 200 kwa ajili ya kutoa msaada wa haraka ili kuokoa maisha ya watu wa Tigray.

Jimbo hilo limetumbukia katika mgogoro baada ya  Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed kupeleka vikosi  mnamo mwezi Novemba ili kuwanyang’anya silaha na kuwakamata viongozi wa TPLF - chama tawala cha hapo awali katika jimbo la Tigray.

Raia waliokimbia mapigano Tigray wakiwasili mji wa ShirePicha: Baz Ratner/REUTERS

Waziri Mkuu Ahmed alietunukiwa tuzo ya amani ya Nobel mnamo mwaka 2019 amesema alichukua hatua hiyo baada ya askari  wa TPLF kuzishambulia kambi za jeshi la serikali kuu.

Tangu wakati huo mgogoro wa Tigray umesababisha athari kubwa kwenye eneo ambalo tayari lilikuwa linakabiliwa na uhaba wa chakula. Shirika la chakula la Umoja wa Mataifa WFP limesema lina wasi wasi kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu wanaohitaji  haraka msaada wa chakula, hata hivyo limeahidi kuchukua kila hatua itakayopasa ili kuwasaidia watu wa jimbo la Tigray.

Msemaji wa shirika la WFP Tomson Phiri amesema hali ya kuyumbayumba katika jimbo la Tigray na hasa kwenye sehemu za mashambani inazuia juhudi la shirika hilo za kutoa misaada. Amesema ni muhimu sana kufikiwa hatua za kusimamisha mapigano pamoja na kuwawezesha watoa misaada wa WFP na washirika wao, ili waweze kuwafikia watu wote wanaohitaji misaada katika jimbo la Tigray, bila ya vizuizi.