Askari wa zamani aliyehukumiwa kwa mauaji ya Rwanda afariki
11 Juni 2023Tharcisse Muvunyi alikuwa katika jeshi la Rwanda wakati Wahutu walio wengi wenye misimamo mikali waliwauwa zaidi ya watu 800,000 kutoka kabila la walio wachache la Tutsi na Wahutu wa misimamo ya wastani katika siku 100. Wakili wake Abbe Jolles amesema Muvunyi alipatikana jana mchana akiwa amefariki bafuni.
Muvunyi luteni kanali wa zamani aliishi katika nyumba salama katika eneo lisilojulikana nchini Tanzania baada ya kuachiwa huru 2012 na akahamia Niger 2021 katika nyumba ya watu saba wengine waliokuwa wameshitakiwa kwa mauaji hayo ya halaiki.
Alikamatwa nchini Uingereza, akahukumiw akifungo cha miaka 15 jela mwaka wa 2010 na akaachiliwa huru miaka miwili baadae baada ya muda aliotumikia.
Alikuwa mgonjwa kwa wiki kadhaa, na wakili wake Jolles akaufahamisha Umoja wa Mataifa kuwa Muvunyi alihitaji matibabu ya dharura Uingereza. Lakini hakupata jibu.