1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UhalifuTanzania

Askari wanawake Afrika kujadili namna kukabiliana na uhalifu

24 Julai 2023

Askari wanawake barani Afrika wameanza mafunzo ya wiki moja nchini Tanzania, wakijikita katika kujiimarisha namna ya kukabiliana na vitendo vya kihalifu, ikiwamo uhalifu unaovuka mipaka na udukuzi katika mabenki.

Emirate Training des rein weiblichen SWAT-Teams der Emirate in Dubai
Picha: Rula Rouhana/REUTERS

Kongamano hilo, lililoandaliwa na shirikisho la kimataifa la polisi wanawake kanda ya Afrika linafanyika katika wakati ambapo dunia ikiwa inashuhudia mapinduzi makubwa ya kiteknolojia yanayotoa msukumo pia vitendo vya kihalifu kufanyika kwa mfumo wa kidigitali.

Wataalamu wa masuala ya ulinzi wa amani na usalamawanasema kiwango cha uhalifu katika nchi za Afrika kimekuwa kikiongezeka kutoka uhalifu wa kupangilia mpaka ule unaotekelezwa na magenge yenye ushawishi kama vile vikundi vinavyojifungamanisha na vitendo vya kigaidi.

Maeneo ya mipakani yamekuwa tena siyo maeneo salama huku wahalifu wakitumia mbinu mbadala kutekeleza vitendo vyao na kisha kuvuka mpaka wa nchi nyingine na kwenda kusaka maficho katika upande wa pili.

Soma pia:HRW: Wanamgambo wanaoungwa mkono na M23 na Rwanda wafanya uhalifu Kongo

Kwa maana hiyo kuwepo kwa kongamano hilo la mafunzo kwa askari wanawake kunatazamwa na wengi kama hatua mujarabu itakayosaidiakusaka jawabu la pamoja katika kuzikabili changamoto za kihalifu zinazojitokeza katika sehemu nyingi za dunia.

Mratibu mwandamizi wa jeshi la polisi, Pili Phope kutoka Tanzania alibainisha kwamba mwishoni mwa kongamano hilo, askari hao wanategemewa kuwa mstari wa mbele kukabiliana na aina zote za kihalifu.

Kongamano hilo ni chachu kwa askari wapya kazini

Likiwa limeanzishwa Oktoba 2007, Shirikisho la kimataifa la polisi wanawake kanda ya Afrika ni taasisi inayofanya kazi kote duniani ikiwaleta pamoja wataalamu wa masuala ya ulinzi wa amani na vyombo vyake kwa shabaha ya kuwa na ajenda moja ya kuzikabili changamoto za kiusalama za dunia.

Wakazi wazungumzia tatizo la "Panya Road"

02:47

This browser does not support the video element.

Kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa kongamano hilo kunatazamwa na wengi kama hatua itakayosaidia kuwapa ujuzi wa kisasa askari wake, ambao wakati mwingine wamekuwa wakitupia lawama kwa namna wanavyoendesha shughuli zao kinyume cha weledi.

Soma pia:Watu 8 wameuwawa katika ufyetuaji risasi Afrika Kusini

Kwa kuzingatia muktadha huo, Mkuu wa chuo cha taaluma ya polisi, Lazaro Mambosasa amewahimiza washiriki wa kongamano hilo kutambua dhima waliyonayo mbele ya jamii, na kuyatumia yale watakayoyapata kama nyenzo ya kukaribisha mabadiliko.

Baadhi ya washiriki wenyewe wanawake wanasema kufanyika kwa kongamano hilo ni kama bahari inayomwaga maji kwenye mito, wakimaanisha kwamba kusanyiko la pamoja la wataalamu kutoka sehemu mbalimbali duniani, ni faraja kwa askari wanaochipukia.

Kongamano hilo linalofanyika jijini Dar es salaam linawaleta pamoja washiriki wanawake kutoka  Kenya, Ethiopia, Zimbabwe, Nigeria, Ghana, Afrika Kusini, Sierra Leone, Botswana, Malawi na Tanzania.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW