1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ASMARA:Waasi wa ARDUF wakiri kuteka raia 4 wa Ulaya

19 Machi 2007

Waasi katika eneo la mbali la Afar lililo karibi na mpaka wa Ethiopia na Eritrea wanakiri kuwateka raia 4 wa Ulaya .Watu hao wane walitekwa wiki iliyopita.Waasi hao waliodai kuwa wa kundi la Afar Revolutionary Democratic Unity Front, ARDUF waliojihami kwa silaha waliyasema hayo walipofanyiwa mahojiano na kituo cha televisheni ya Kitaifa cha Eritrea.Kituo hicho kilionyesha pia picha za kwanza za mateka hao walipoachiwa huru.

Kwa mujibu wa msemaji wa kundi hilo la ARDUF lengo la kuwakamata watu hao lilikuwa kujitangaza baada ya serikali kueneza taarifa kuwa kundi hilo halipo tena.

Kwa upande mwingine ripoti hiyo haikuangazia suala la mateka wanane wa Ethiopia waliotekwa katika eneo la jangwani kaskazini mashariki mwa Ethiopia ambao bado hawajulikani waliko.Kulingana na nchi ya Eritrea watu hao walikamatwa na kundi la waasi la ARDUF linalopinga utengano katika jamii ya Afar katika nchi za Ethiopia,Eritrea na Djibouti.

Eritrea inakanusha madai hayo yaliyotolewa na nchi ya Ethiopia kuwa ilipanga njama hiyo ya utekaji.Nchi za Ethiopia na Eritrea bado zinahasimiana kufuatia mzozo wa mpaka tangu mwaka 2000.