Assad atapata ujumbe ? Waulize Warusi na Iran
15 Aprili 2018Utawala wa Trump uliweka wazi kwamba mashambulizi dhidi ya mpango wa silaha za sumu wa Syria yalikuwa na lengo moja: Kumzuwia rais wa Syria Bashar al-Assad kutumia silaha kama hizo tena hapo baadaye kama alivyofanya, Marekani na mataifa mengine yamesema, hivi karibuni katika mji wa Douma.
Mashambulio ya siku ya Ijumaa usiku yalikuja mwaka mmoja baada ya Marekani kushambulia utawala wa Assad kwa namna hiyo baada ya Syria kudaiwa kufanya shambulio baya la gesi ya sumu katika mji wa khan Sheikhoun. Mara hii , hata hivyo, Marekani haikuchukua hatua peke yake, na yenyewe pamoja na Ufaransa na Uingereza, zilifanya mashambulizi mengi zaidi kuliko mwaka mmoja uliopita.
Hatua hiyo iliyoongozwa na Marekani , iliyoelezwa kama shambulio moja kubwa, lilikuwa kilele cha hatua zenye vurumai kubwa kuelekea hatua za kuingilia kati ambazo zilianzia, kama ilivyokuwa kawaida kwa Marekani , kwa rais kuandika katika ukurasa wa Twitter. Katika ujumbe huo, Trump aliahidi hatua za haraka na kali za kijeshi , akimshutumu Assad na kuzikejeli Urusi na Iran. Maandishi hayo ya Twitter yalizusha tahadhari kimataifa juu ya shambulio ambalo litatokea katika moja kati ya maoneo yenye matatizo na kuwaacha maafisa wa Marekani wakijaribu kutafuta majibu.
Wakati shambulio hilo lilipotokea , siku kadhaa baada ya Trump kutoa muda wa awali, kulikuwa na washirika wawili na mtazamo wa kupunguza malengo ya mashambulizi hayo. Kwa wachunguzi wengi , hatua hizo za kijeshi zilionekana zaidi kama jibu lililowekewa mipaka zaidi kuliko shambulio kubwa ambalo lilielezwa hapo kabla na Trump. Hali hiyo imesababisha maswali kadhaa.
Je Assad atapata ujumbe na kujizuwia kutumia silaha za sumu ?
"Sina shauku," amesema Ryan Crocker , balozi wa zamani wa Marekani nchini Syria, ambae pia alifanyakazi kama mjumbe wa Marekani nchini Iraq, Afghanistan na Pakistan. "Tulifanya kitu kama hicho mwaka mmoja uliopita katika kiwango kidogo. lakini mashambulizi haya hayatafanya uharibifu wa kudumu kwa uwezo wa Assad wa kutumia silaha za sumu hapo baadaye ama kitu kingine zaidi.
"Hilo ni swali ambalo linabaki wazi," amesema Philip Breedlove, kamanda wa zamani wa NATO na jeshi la Marekani barani Ulaya. "Kumbuka kwamba mhalifu huyu, kiongozi huyu zimwi wa Syria , anapata uungwaji mkono na uwezo na uungwaji mkono wa kisiasa kutoka Urusi na Iran."
Wakati ni vigumu kutabiri jibu la Assad, kubadili utaratibu wake utahitaji hatua ambazo zinatishia msingi halisi wa utawala wake, amesema Mona Yacoubian , msomi raia wa Syria katika taasisi ya amani ya Marekani. Katika hali hiyo , mashambulizi haya huenda ni madogo sana kutimiza lengo.
Wataalamu wote watatu wamezungumzia ushawishi wa Urusi na Iran katika utawala wa Assad. "Kumbuka kwamba Bwana Assad binafsi hana uwezo wa mambo yote haya ambayo yanatokea karibu yake," amesema Breedlove. "Anapata uwezo, anapewa nguvu na kuhimizwa na Urusi na Iran."
Kwa upande wake viongozi wa mataifa ya kiarabu , akikosekana rais Bashar al-Assad wa Syria wamekutana nchini Saudi Arabia kwa ajili ya mkutano unaofanyika leo wakati mataifa yenye nguvu dunaini yakipambana kuhusu Syria na hali ya wasi wasi ikiongezeka kati ya Riyadh na Tehran.
Saudi Arabia inataka kupatikana msimamo mkali , na wa pamoja dhidi ya hasimu yake mkubwa Iran katika mkutano huo wa kila mwaka wa mataifa 22 wanachama wa Jumuiya ya mataifa ya Kiarabu, Arab league.
Mataifa hayo makubwa katika eneo la mashariki ya kati, yanapigana vita nchini Syria, na katika eneo la kusini mwa Saudi Arabia katika nchi jirani ya Yemen, yakiunga mkono pande zinazopingana nchini Iraq na Lebanon.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mahariri: John Juma