1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Muasisi wa WikiLeaks hatimae aondoka London alikokuwa jela.

25 Juni 2024

Muasisi wa mtandao wa ufichuzi wa siri za serikali za mataifa,Julian Assange aachiwa huru kutoka gereza la Berlmash baada ya jaji wa Marekani kusaini makubaliano ya kisheria na mshtakiwa huyo.

Großbritannien | Julian Assange
Picha: @wikileaks" via X/Handout via REUTERS

Mwasisi wa mtandao wa WikiLeaks, uliotumika  kufichuwa siri kubwa kubwa za serikali za mataifa mbali mbali duniani, Julian Assange hatimae ameachiwa huru kwa dhamana, Jumatatu.

Assange aliachiwa huru kwa dhamana kutoka jela yenye ulinzi mkali ya  Kusini Mashariki mwa London jana Jumatatu.

Mkewe Stella Assange akionekana kushusha pumzi alisema hivi sasa mumewe ni mtu huru,  baada ya jaji wa Marekani kusaini kuridhia makubaliano ya kihistoria ya kisheria kati ya upande wa Mashtaka ambayo ni Marekani na mshtakiwa.

Chini ya makubaliano hayo Assange anatarajiwa kukubali mashtaka katika mchakato unaotarajiwa kufanyika siku ya Jumatano katika eneo la visiwa vya Northern Mariana  ambalo liko chini ya himaya ya Marekani katika eneo la bahari ya Pasifiki.

Julian Assange awasili BangkokPicha: Sakchai Lalit/AP Photo/picture alliance

Stella Assange anasema chini ya makubaliano hayo ya kisheria mumewe atakubali kuwa na hatia ya shtaka moja tu,ambalo linahusiana na  kitendo cha udukuzi kujipatia taarifa kuhusu ulinzi wa taifa na kuzisambaza taarifa hizo.

Stella Assange amesema hatimae huu ndio mwisho wa safari ndefu ya mapambano ya kisheria ya mumewe ambaye jana Jumatatu baada ya kuachiwa kwenye gereza la  Berlmash,nchini Uingereza alifanikiwa kuchukuwa ndege kutoka London kuelekea Bangkok na hatiamae, Saipan mji mkuu wa visiwa vya Northern Mariana, katika safari iliyojawa na hisia nyingi.

Mwasisi huyo wa mtandao wa WikiLeaks Julian Assange,mwenye umri wa miaka 52 na raia wa Austarlia, amekaa  jela kwa miaka mitano akipambana kupinga kupelekwa Marekani,nchi ambayo ilitaka kumshtaki kwa kufichuwa nyaraka za siri za jeshi la taifa hilo.

Maandamano ya kumuunga mkono Assange -LondonPicha: Lucy North/PA/AP/picture alliance

Waziri mkuu wa Australia Anthony Albanese akizungumzia juu ya kuachiliwa kwa dhamana kwa Assange kutoka jela ya Uingreza alikuwa na haya ya kusema.

"Serikali bila shaka inatambuwa kwamba raia wa Australia bwana Julian Assange anakabiliwa na mchakato wa kisheria uliopangwa na  Marekani. Wakati tukiikaribisha hatua hii mpya tunatambuwa kwamba hii michakato ni muhimu na ni tete.Na kwasababu mchakato unaendelea,sio busara kuzungumzia hili''

Stella Assange,mke wa Julian AssangePicha: REUTERS

Kwa mujibu wa mkewe Assange kitu muhimu katika makubaliano ya kisheria yaliyofikiwa ni kwamba muda aliokaa jela mumewe unazingatiwa  na ikiwa mchakato utakaoendeshwa Jumatano utakwenda vizuri mumewe atakuwa huru kabisa.