1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Assange kuzungumza na dunia

19 Agosti 2012

Muasisi wa tovuti iliyofichua nyaraka za siri za kidiplomasia duniani kote ya Wikileaks Julian Assange,anatarajiwa kuzungumza na vyombo vya habari leo(19.08.2012) kutoka katika ubalozi wa Ecuador mjini London.

A protestor holds a poster of Wikileaks founder Julian Assange outside Ecuador's embassy in London August 17, 2012. REUTERS/Neil Hall (BRITAIN - Tags: POLITICS CRIME LAW MEDIA)// eingestellt von nis
Ecuador yamkingia kifua AssangePicha: Reuters

Lakini anakabiliwa na kitisho cha kukamatwa iwapo atachomoza mguu wake nje ya jengo anamopatiwa hifadhi.

Wakati maafisa wa polisi wakijiweka tayari kumkamata , Assange anapaswa kutafuta njia ya kuweza kuzungumza na dunia bila ya kuweka mguu wake nje ya jengo hilo la ubalozi, na kuzusha uwezekano wa yeye kulazimika kuzungumza kutoka katika baraza ya ghorofa ya jengo hilo, ama kujitokeza dirishani.

Wikileaks wako kimya

Wikileaks imekaa kimya juu ya mbinu atakazotumia Assange wakati akipanga kuzungumza na vyombo vya habari mchana wa leo, huku msemaji wa tovuti hiyo maarufu, Kristinn Hrafnsson aliliambia shirika la habari la AFP kuwa kile kidogo anachokifahamu hakiwezi kujadiliwa kutokana na "sababu za kiusalama".

Lakini wizara ya mambo ya kigeni ya Uingereza imeonya kuwa ngazi za jengo la ubalozi huo zinachukuliwa kuwa eneo la ardhi ya Uingereza, wakati polisi imesema kuwa maafisa wa jeshi hilo watachukua hatua zinazostahili, iwapo atapiga hatua moja tu nje ya jengo la ubalozi huo.

Assange mwenye umri wa miaka 41, alikimbilia katika ubalozi huo Juni 19 kuepuka kupelekwa nchini Sweden ambako anatakiwa kwa mahojiano kuhusiana na madai ya vitendo vinavyokwenda kinyume na tendo la ngono.

Julian Assange anayetakiwa na Marekani

Wahofia atapelekwa Marekani

Waungaji mkono wa raia huyo wa Australia ambaye alikuwa zamani anajishughulisha na utundu wa kujipenyeze katika tovuti mbali mbali kwa siri katika mtandao wa internet, na ambaye alipatiwa hifadhi ya kisiasa na serikali ya Ecuador siku ya Alhamis, wiki iliyopita, wanaamini kuwa mara atakapofikishwa Sweden anaweza kupelekwa nchini Marekani.

Machapisho ya Wikileaks ya nyaraka kadhaa za siri za serikali , yameikasirisha serikali ya Marekani na waungaji wake mkono wanahofia kuwa anaweza kushtakiwa kwa madai ya ujasusi na kukabiliwa na adhabu ya kifo.

Wikileaks imetangaza katika tovuti ya twitter siku ya Jumamosi kuwa mwanasheria maafuru wa Uhispania Baltasar Garzon atazungumza nje ya ubalozi huo leo.

Garzon , anayefahamika kwa kumfuatilia dikteta wa zamani wa Chile Augusto Pinochet, anakisaidia kikosi cha wanasheria wanaomtetea Assange. Licha ya Ecuador kumpatia hifadhi Assange, waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza William Hague amesema kuwa Uingereza haina chaguo ila kujaribu kumpeleka kule anakotakiwa.

Balozi ni ardhi ya nchi husika

Kwa misingi ya utaratibu wa kidiplomasia , balozi zinachukuliwa kuwa ardhi ya nchi husika inazoziwakilisha na nchi mwenyeji inahitaji ruhsa kuingia katika eneo hilo.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza William HaguePicha: AP

Uingereza imeikasirisha Ecuador kwa kuonyesha kuwa inaweza kuondoa hadhi ya kidiplomasia katika sheria ya mwaka 1987, ambayo inasema kuwa inairuhusu kuondoa hadhi ya kidiplomasia ya ubalozi katika ardhi ya Uingereza na kuingia ndani ya jengo hilo kumkamata Assange.

Maafisa kiasi ya kumi na waungaji mkono kiasi wa Assange walikuwa nje ya ubalozi huo siku ya Jumamosi,(18.08.2012).

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe

Mhariri: Bruce Amani

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW