1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaUlaya

AstraZeneca: Madaktari wagundua chanzo cha mvilio wa damu

21 Machi 2021

Wanasayansi katika hospitali ya mafunzo ya chuo kikuu cha Greifswald wanadai k´wamegundua kisababishi cha kuganda kwa damu miongoni mwa watu wachache waliopokea chanjo ya Astrazeneca.

Weltspiegel 19.03.2021 | Corona | Impfstoff AstraZeneca, Europa
Picha: Alexandre Marchi/Photopqr/L'Est Républicain/picture alliance

Watafiti kutoka hospitali ya mafunzo ya chuo kikuu cha Greifswald kaskazini mwa Ujerumani wamesema Ijumaa kuwa wamegundua chanzo cha kuganda kwa damu kusiko kwa kawaida miongoni mwa baadhi ya wapokeaji wa chanjo ya virusi vya corona kutoka AstraZeneca, kiliripoti kituo cha utangazaji cha umma cha Norddeutscher Rundfunk (NDR).

Uchunguzi umeonesha namna chanjo hiyo ilivyosababisha mvilio usio wa kawaida kwenye ubongo katika idadi ndogo ya wagonjwa. Ugunduzi huo unamaanisha kwamba tiba makhsusi inaweza kutolewa kwa wale wanaokabiliwa na mvilio sawa, kwa kutumia dawa ya kawaida sana.

Soma pia: Mataifa ya Ulaya kuanzisha tena matumizi ya AstraZeneca

Mafanikio hayo yalikuwa matokeo ya ushirikiano kati ya hospitali ya Greifswald, mamlaka ya afya ya jimbo - Taasisi ya Paul Ehrlich (PEI), pamoja na madaktari wa nchini Austria - ambako muunguzi alifariki kutokana na mvilio katika ubongo baada ya kudungwa na chanjo ya AstraZeneca.

Watafiti wamesisitiza kwamba tiba itawezekana tu miongoni mwa wagonjwa ambako mgando wa damu unaonekana, kuliko kuwa kama tiba ya kuzuwia. Taarifa hizi zimetolewa kwa hospitali kote barani Ulaya.

Daktari Natascha Kempkes kutoka Berlin akimdunga chanjo Beatrix Mengen katika uwanja wa zamani wa ndege wa Tegel kwa kutumia chanjo ya AstraZeneca.Picha: Soeren Stache/dpa/picture alliance

Dalili kama vile maumivu ya mara kwa mara ya kichwa, kisunzi au kupungua kwa uwezo wa kuona zinazodumu kwa zaidi ya siku tatu baada ya kuchanjwa zinahitaji uchunguzi zaidi wa kitabibu, kwa mujibu wa chama cha utafiti cha Ujerumani kwa ajili ya mvilio, katika taarifa kuhusu ugunduzi huo wa karibuni. 

Ugunduzi wa Greifswald haujachapishwa bado katika jarida ya kisayansi na hivyo haujapitiwa na wataalamu huru. Taasisi ya Paul Ehrlich nchini Ujerumani sasa inapitia kazi hiyo ya wanasayansi.

Soma pia: Madaktari Ujerumani waonya usitishaji chanjo ya AstraZeneca

Chanjo ya AstraZeneca yarudi Ulaya


Ujerumani, pamoja na mataifa kadhaa ya Umoja wa Ulaya, yalisitisha matumizi ya chanjo ya AstraZeneca siku ya Jumatatu kufuatia ripoti za mvilio usio wa kawaida wa damu.

Siku ya Alhamisi, mamlaka ya usimamizi na udhibiti wa dawa ya Umoja wa Ulaya EMA, ilisema hakukuwa na uhusiano uliyothibitishwa kati ya chanjo na mvilio wa damu, kwa msingi wa taarifa walizokuwa nazo. Walibanisha pia kwamba manufaa ya chanjo hiyo yanazidi uwezekano wowote wa hatari.

Katika kujibu muongozo huo mpya, Ujerumani ilipanga kuanza tena kutoa chanjo hiyo ya Uingereza na Sweden kuanzia Ijumaa. Kufikia Alhamisi, Ujerumani ilikuwa imetoa zaidi ya dozi milioni 10 za chanjo ya covid-19, ikiwemo ya AstraZeneca.