1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Athari ya sumu ya madini ya risasi kwenye rangi

9 Februari 2026

Kwa miaka mingi, madini ya risasi yalitumika kwenye rangi ili kuongeza uimara na kung'aa kwa rangi. Hata hivyo tafiti za kisayansi zimebaini kuwa risasi ina madhara makubwa kwa afya, hasa kwa watoto wadogo na wajawazito.

Kabul, Afghanistan 2021 | Kiwanda cha rangi Afghanistan
Kasi ya kutekeleza kanuni kali za kusimamia madini ya risasi kwenye rangi yapaswa kuongezwaPicha: Sajjad Hussain/Getty Images/AFP

Licha ya kupigwa marufuku katika nchi nyingi, madini ya risasi bado yanaendelea kupatikana kwenye baadhi ya rangi zinazouzwa sokoni. Mwishoni mwa mwezi Januari mwaka 2026, wajumbe wa serikali kutoka nchi 25 za Afrika walikutana jijini Nairobi, Kenya, katika mkutano wa siku mbili uliojadili hatari na kuendeleza juhudi za kudhibiti matumizi ya madini ya risasi hasa kwenye rangi na bidhaa nyingine.

Katika nchi nyingi za Afrika, kanuni kuhusu madini ya risasi bado ni hafifu au hazitekelezwi vizuri. Hii inaongeza matatizo makubwa ya afya, hasa kwa watoto, ambao wanaweza kupumua chembechembe za madini ya risasi kupitia vumbi, rangi zinazotumika kwenye majengo, na kwenye vyanzo vingine.

Peter Kaigwara, Mkurugenzi wa ufuatiliaji wa soko katika Mamkala ya Kudhibiti Viwango nchini Kenya, KEBS, anasema ni lazima ufanyike ufuatiliaji wa mara kwa mara ili kubaini kwa uhakika kiwango cha utii wa sheria kote nchini.

Kiwango cha kufuatilia sampuli zinazokusanywa

''Changamoto ya kubaini kiwango cha utii wa sheria ni kwamba ufuatiliaji unategemea idadi ndogo ya sampuli unazochukua kutoka sokoni. Kwa hivyo siwezi kukupa asilimia ya utii kote nchini, kwa sababu upimaji unategemea idadi ya sampuli zilizokusanywa,'' alifafanua Peter.

Madini ya risasi yanaweza kusababisha madhara makubwa ikiwa hayadhibitiwi vizuri. Baadhi ya athari kwa afya ya watoto ni uwezekano wa kupata matatizo ya ukuaji wa ubongo, upungufu wa fahamu, matatizo ya kusoma na kuandika.

Kiwango cha risasi mwilini kinaweza kuathiri maendeleo ya utambuzi na kusababisha matatizo ya kiafya ya kudumu. Kwa watoto, madini ya risasi yanaweza kuingia mwilini kupitia vumbi la rangi iliyochakaa au vipande vidogo vya rangi vinavyong'oka kutoka ukutani.

Kanuni kuhusu madini ya risasi bado ni hafifu AfrikaPicha: Mahila Housing Trust

Kwa watu wazima inaweza kusababisha athari kwenye moyo, maumivu ya figo, uchovu wa kudumu, mfumo wa homoni na matatizo ya uzazi. Kwa kina mama wajawazito madini ya risasi huweza kumuathiri mtoto aliye tumboni na kusababisha mimba kuharibika au mtoto kuzaliwa na changamoto za kiafya.

Kenya inakabiliwa na changamoto ya vifo vya watoto wachanga. Kulingana na takwimu za Wizara ya Afya, watoto 134,000 huzaliwa kabla ya wakati kila mwaka nchini Kenya, huku watoto wachanga 33,600 wakifariki kila mwaka kutokana na matatizo yanayotokana na kuzaliwa kabla ya wakati. Wadau wanahimiza kutilia mkazo ushirikiano wa kitaifa na kikanda, kanuni madhubuti, na hatua za afya ya umma ili kulinda jamii, hasa watoto dhidi ya athari za sumu ya madini ya risasi.

Licha ya hatari hizi, bado kuna rangi zinazouzwa bila taarifa sahihi kuhusu viwango vya madini hayo ya risasi. Wataalamu wa afya na mazingira wanaihimiza serikali kuimarisha ukaguzi wa rangi zinazoingizwa na kutengenezwa nchini, kama anavyoeleza Purity Kamau, mkurugenzi wa kemikali na madini katika Wizara ya Uwekezaji ya Kenya.

Umuhimu wa viwanda 

''Tunahitaji kuwa na sera na kanuni zinazofaa. Hii itatuwezesha kufuatilia masuala hayo, kuhakikisha kuwa taasisi husika zinayashughulikia ipasavyo, na pia kuhakikisha kuwa viwanda, hasa wazalishaji, wanaelewa kile kinachopaswa kufanywa,'' alibainisha Purity.

Viongozi wa Afrika anayataka mataifa ya kikanda kuongeza kasi ya utekelezaji wa kanuni kali za kusimamia madini ya risasi kwenye rangi na bidhaa zinazoweza kusababisha sumu ya madini hayo, kuunganisha mafunzo na utafiti wa pamoja na kubadilishana uzoefu na kujenga uwezo wa kiufundi kwa watendaji wa serikali na watoa sera.

Vile vile wanasisitiza kuunda mipango ya kitaifa ya utekelezaji wa kanuni ili kulinda afya ya watoto na jamii kwa ujumla. ''Ili kuzuia bidhaa zisizo salama kuingizwa sokoni, wanahitaji sera hizo na taasisi husika kuhakikisha kuwa usalama wa rangi unashughulikiwa ipasavyo,'' alifafanua Purity.

Wananchi pia wanashauriwa kusoma maelezo yanayoandikwa kwenye makopo ya rangi kabla ya kununua, kuepuka rangi zisizo na cheti chenye ubora, na kuhakikisha nyumba wanazoishi, hasa zenye watoto, hazina rangi zilizochakaa au kuanza kupukutika.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW