Athari za Covid miaka miwili baada ya kutangazwa kuwa janga
11 Machi 2022Ugonjwa wa Covid-19 umegharimu maisha ya zaidi ya watu milioni sita duniani kote. Wataalamu wanakadiria kuwa, idadi hiyo huenda ikawa mara mbili au mara nne zaidi ya iliyoripotiwa huku vifo vingi vikiripotiwa zaidi miongoni mwa wazee.
Na kwa wale walionusurika kifo baada ya kuugua, wanaendelea kupambana na athari za muda mrefu za ugonjwa huo ambao aghalabu hushambulia mapafu na wengine, wamewachwa na ulemavu wa kudumu kutokana na ugonjwa wa Covid-19.
Covid-19 imeathiri sekta ya elimu
Ama kwa upande wa elimu, ugonjwa wa Covid-19 umezima ndoto za wanafunzi wengi. Elimu ya takriban wanafunzi bilioni mbili imekatizwa, aidha kwa muda ama wengine wasiobahatika safari yao ya elimu imefika mwisho ghafla.
Shule kadhaa zililazimika kufungwa na kusitisha elimu kwa mamilioni ya wanafunzi hasa wasichana na watoto maskini. Hali hiyo iliwasukuma wasichana wengi ndani ya shimo la ndoa za mapema, ilhali wengine walianza ulezi au uzazi kabla ya kubaleghe.
Soma pia: Oxfam: Mabilionea watajirika maradufu wakati wa Covid-19
Si hayo tu, janga la Covid-19 limekuwa sumu kwa maendeleo. Takwimu zinaonyesha kuwa watu nusu bilioni walilazimishwa kuingia katika umaskini, na wale waliokuwa maskini tayari, hali yao ya umaskini ilizidi kuwa mbaya na mpaka sasa, janga hilo limesababisha kudorora kwa uchumi duniani kote.
Janga la Covid-19 bado halijakwisha. Tunapoingia mwaka wa tatu wa janga hili la ulimwengu, mwanya wa ukosefu wa usawa umezidi kupanuka. Mfano hai ni katika usambazaji wa chanjo dhidi ya virusi vya Corona.
Nchi maskini zimewachwa nyuma katika zoezi la chanjo
Miezi kumi na tano baada ya shirika la afya duniani WHO kutoa idhini ya chanjo ya kwanza dhidi ya Covid-19, kumetokea tofauti kubwa katika usambazaji wa chanjo hiyo. Ni dhahiri kuwa zipo sehemu ambazo watu wanapokea dozi ya tatu au hata ya nne ilhali zaidi ya asilimia 85 ya watu wanaoishi katika nchi za kipato cha chini bado wanasubiri angalau dozi ya kwanza tu za kuwapa matumaini ya kupambana na ugonjwa wa Covid-19.
Licha ya kutolewa kwa chanjo, mkoko ndio mwanzo unaalika maua katika maeneo ya New Zealand, Korea Kusini, Hong Kong na Vietnam. Maeneo hayo yameorodhesha idadi kubwa ya maambukizo mapya ya ugonjwa wa Covid-19 hivi karibuni. Dunia bado inajikuna kichwa, ni nini kilipaswa kufanyika tofauti kupambana na janga hili?
Soma zaidi:Aina mpya ya kirusi cha Omicron yaripotiwa
Utafiti wa Human Rights Watch umeangazia miongoni mwa sababu za kwanini janga la Covid-19 limeonekana kukosa mwarobaini. Mojawapo ya sababu kuu ni kushindwa kwa serikali kulinda haki za binadamu pamoja na kutumia janga la Covid kama mbinu za kupanua mamlaka na hatimaye kuzima upinzani.
Human Rights Watch inapendekeza mbinu mbadala za kuzingatiwa iwapo kweli dunia inataka suluhu ya kudumu kupambana na jinamizi hili la Covid-19.