1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Athari za Kimbunga Mangkhut bado ni Kubwa

Admin.WagnerD17 Septemba 2018

Waokoaji nchini Ufilipino wameendelea na juhudi za uokoaji wakitumia mapauro na mikono kufukua vifusi venye mawe wakijaribu kutafuta watu wanaokisiwa kufunikwa na maporomoko ya udongo yaliyotokana na kimbunga Mangkhut.

Philippinen Taifun Mangkhut
Picha: picture-alliance/dpa/AP/A. Favila

Wakoaji tayari wamefanikiwa kupata miili 11 kutoka kwenye eneo la Itogon huku wengine wengine wakihofiwa kuwa bado wamefukiwa na matumaini ya kuwapata wakiwa hai yamefifia.

Familia zilizojawa majonzi zimeoneka zikikusanyika kwenye ubao mweupe ulio na orodha ya majina ya waliofariki dunia na ambao bado hawajapatikana huku wengine wakikagua  miili iliyopatikana kujaribu kutafuta wapendwa wao saa  48 baada ya kimbunga Mangkhut kulipiga eneo la kaskazini ya kisiwa kikubwa nchini Ufilipino cha Luzon.

Mvua zilizotokana na Kimbunga Mangkhut zilisababisha kudhoofika kwa udongo na kusababisha  maporomoko yaliyowafunika wachimba madini waliokuwa kiasi nusu kilometa chini ya ardhi.

Kutokana na kuharibiwa vibaya kwa barabara kulikozuia uwezekano wa kutumia vifaa vikubwa kama tingatinga, wanajeshi, polisi na wachimbaji   wengine wametumia chepe kutengeneza njia ya kuondoa maji kutoka eneo la tukio kurahisisha juhudi za uokozi.

Maelfu ya waokoaji wakiwa wamejipanga mstari wameonekana wakipokeza mawe, mabaki na matawi ya miti kutoka kwenye eneo la utafutaji wahanga wa maporomoko ya udongo kwenye mji wa Itogon.

Matumaini ya kuwapata walio hai yanafifia

Picha: picture-alliance/dpa/AP/A. Favila

Meya wa mji wa Itogon katika jimbo la Benguet miongoni mwa maeneo yaliyoathiriwa vibaya na kimbunga hicho cha siku ya jumamosi amesema hakuna tena matumaini kuwa watu wanaohofiwa kufukiwa na maporomoko ya udongo watapatikana wakiwa hai lakini waokoaji wataendelea na kazi ya kuchimba kifusi.

Kiongozi huyo amesema inakadiriwa watu 40 hadi 50 walikuwepo kwenye eneo hilo wakati maporomoko yalipotokea.

Mangkhut, kimbunga kikubwa kabisa kwa mwaka huu kiliipiga Ufilipino mwishoni mwa juma kikisababaisha mvua kubwa na upepo mkali uliong'oa nguzo za umeme na kufumua paa za nyumba .

Mamlaka nchini ufilippino zimesema watu 65 wamethibitishwa kufariki dunia wengi wao wakiwa waliofukiwa na maporomoko ya udongo.

Rais wa Ufilipino Rodrigo Duterte amerudia wito wake wa kutaka kufungwa kwa migodi yote nchini humo kutokana na maporomoko hayo ya ardhi saa chache baada ya waziri wake kusitisha shughuli zote za uchimbaji mdogo wa madini kwenye eneo la Cordillera lenye utajiri wa dhahabu ambapo maporomoko ya udongo yamewaua watu 24.

Duterte ameikosoa mara kadhaas ekta ya madini akisema athari zake kwa mazingira zinapindukia faida yoyote kwenye uchumi wa taifa lake.

Hali ya kawaida imeanza kurejea

Picha: Reuters/J. Lee

Hadi jumatatu kimbunga Mangkhut kilikuwa kinaipiga pwani ya kusini mwa China pamoja na majimbo ya Guangdong, Guangxi na Hainan,wakati mvua kubwa na upepo mkali ukatarijiwa kuendelea siku ya  jumanne.

Shughuli za kawaida zinarejea taratibu katika eneo lililopigwa vibaya na kimbunga hicho la kusini mwa pwani ya china ambapo majengo marefu yalitikiswa, hoteli za pembezoni mwa fukwe kufurika na madirisha yalivunjwa na kupeperushwa kwa upepo.

Usafiri wa treni, ndege na vivuko ulifunguliwa kwenye mji wa Macau wakati Mjini Hong Kong zoezi la kusafisha mji ikiwemo kuondoa miti iliyoanguka na mabaki mengine inaendelea baada ya mji huo muhimu wa kibiashara kupigwa vikali na kimbunga hicho siku ya Jumapili.

Mwandishi: Rashid Chilumba/AFP/RTRT/
Mhariri: Mohammed Khelef

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW