Mabadiliko ya tabianchi ni changamoto kwa amani Somalia
23 Oktoba 2019Ripoti hiyo imesema mabadiliko ya tabianchi yanaongeza changamoto zinazochangia kuimarika kwa makundi ya itikadi kali.
Miongo mitatu ya mzozo nchini Somalia imelipeleka taifa hilo kukabiliwa na ongezeko la ukame mkali. Matokeo ya mabadiliko ya tabianchi na yanayohusiana na hali ya hewa pia yanaongeza shinikizo kwenye mifumo iliyoelemewa ya kiutawala na mahakama ya nchini humo.
Kulingana na ripoti hiyo kitisho hiki ni kikubwa dhidi ya mchakato wa ujenzi wa taifa hilo la Somalia, lakini pia kizuizi kikubwa kwa ujumbe wa amani wa Umoja wa Mataifa nchini humo, UNSOM katika kutekeleza majukumu yake kwa mafanikio.
Ripoti hiyo pia imegundua kuongezeka kwa visa vya mafuriko, ukame na njaa, kumeruhusu wanamgambo wa al-Shabaab kutumia mwanya huo kujionyesha kama wanaoweza kuisaidia jamii kuliko UNSOM. Huu ni mkakati wao mpya, tofauti na awali ambapo waliwazuia watu kuondoka kwenye maeneo yao na kuomba misaada kwenye maeneo yanayodhibitiwa na serikali.
Mkakati huu wa sasa umewasaidia kuongeza ushawishi na jamii kuwachukulia kama wao ni bora zaidi ya ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa.
Al Shabaab huchukuliwa kama mtoaji bora wa huduma kwa sababu ni kundi linalostahimili athari za mabadilio ya tabianchi na UNSOM huonekana kuwa dhaifu katika kuliwekea udhibiti. Hilo limewawezesha kupata uhalali kutoka kwa raia.
Aidha watu wengi huchagua kwenda katika mahakama za al-Shaabab, kwa madai kwamba hazina urasimu, na maamuzi yao hutekelezwa kwa sababu al-Shabaab bado ina uwezo wa kutumia nguvu. Bila shaka hiki ni kitu ambacho kinahujumu mchakato mzima wa ujenzi wa taifa, kwa mujibu wa afisa mmoja wa UNSOM aliyenukuliwa kwenye ripoti hiyo.
Ripoti hiyo imesema asilimia 94 ya jamii ya kuhamahama nchini humo, hasa wafugaji wanaishi katika umasikini mkubwa. Mabadiliko ya tabianchi yamesababisha wafugaji kuhamia kwenye maeneo mapya wakisaka malisho hatua ambayo mara nyingine huwaingiza kwenye mizozo na wakulima.
Athari za mabadiliko hayo pia, zimechangia ongezeko la watu ambao hukimbia makazi yao na hadi sasa hawajulikani walipo. Al-Shabaab hutumia fursa hiyo kuwakamata na kuwapa mafunzo ya kijeshi, hali inayosababisha kubadilika kwa muundo wa idadi ya watu na hata maeneo ya kikabila.
Katika nyakati nyingine mabadiliko haya hufifisha utekelezaji wa makubaliano ya kugawana madaraka ya ndani, lakini pia kudhoofisha juhudi za Umoja wa Mataifa za kujenga taasisi za kiutawala nchini humo.
Hata hivyo, UNSOM imekuwa ikifanya jitihada kadha wa kadha katika kukabiliana na ongezeko la athari za mabadiliko ya tabianchi. Hatua hizo ambazo ni pamoja na kuanzishwa kwa vituo vya kuratibu operesheni za kupambana na ukame pamoja na uteuzi wa mshauri wa usalama wa mazingira zinadhihirisha maono ya ujumbe huo ya muda mrefu na mfupi katika jamii za Kisomali.