Athari za tangazo la ushuru wa Rais Trump zaanza kujitokeza
3 Februari 2025Rais wa Marekani, Donald Trump aliamsha tena mvutano wa kibiashara siku ya Jumamosi baada ya kutangaza mpango wake wa kupandisha ushuru kwa baadhi ya mataifa, hatua iliyozua wasiwasi kuhusu athari zake kwa uchumi wa mataifa hayo na dunia kwa ujumla.
Akiwa hata hajamaliza wiki mbili madarakani, Rais wa Marekani, Donald Trump, ameanzisha upya mvutano wa kibiashara kwa kutangaza ongezeko la ushuru kwa bidhaa zinazoingizwa kutoka Canada, Mexico, na China. Hatua hii inatarajiwa kuwa na athari kubwa kwa biashara na uchumi siyo tu wa mataifa hayo matatu, bali pia kwa Marekani yenyewe.
Umoja wa Ulaya nao uko hatarini
Trump ametangaza kuwa bidhaa kutoka Canada na Mexico zitalipishwa ushuru wa asilimia 25, huku zile kutoka China zikitozwa asilimia 10. Akitetea uamuzi huo, msemaji wa Ikulu ya White House, Karoline Leavitt, amesema haya ni miongoni mwa ahadi ambazo Trump alitoa na sasa anazitekeleza, hivyo si jambo jipya.
Kana kwamba hiyo haitoshi, Trump aliwaambia waandishi wa habari jana Jumapili, akiwa katika kambi ya kijeshi ya Andrews huko Maryland, kwamba Umoja wa Ulaya nao unapaswa kujiandaa kwa hatua kama hizo. Alidai kuwa Marekani imekuwa ikitafunwa kiuchumi kutoka kila upande duniani, na sasa ni wakati wa kulinda maslahi yake.
SB: Rais Donald Trump: Tuna upungufu wa zaidi ya dola bilioni 300. Hawachukui magari yetu, hawachukui bidhaa zetu za kilimo, hawachukui chochote na tunachukua kila kitu kutoka kwao, mamilioni ya magari, chakula kingi na bidhaa za kilimo.
Jana Jumapili, aliporejea kutoka Florida, Trump alitishia kupanua ushuru kwa maeneo mengine zaidi, akisisitiza kuwa ataweka ushuru kwa bidhaa zinazoingizwa Marekani. Miongoni mwa mataifa aliyoyataja ni Uingereza, ambayo tayari imejiondoa kwenye Umoja wa Ulaya. Hata hivyo, aliongeza kuwa atafanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, ambaye alimuelezea kama mtu wanayeweza kuelewana vizuri.
Hatua ya Trump ya kuweka ushuru kwa baadhi ya mataifa, ambayo alitia saini Jumamosi akiwa mapumzikoni Florida, si tu kwamba imezua hofu na mtikisiko wa kiuchumi, bali pia inahatarisha kuvunja ushirikiano wa kibiashara wa miongo kadhaa kati ya Marekani na washirika wake, huku ikizidisha mvutano na China.
Trump awaonya raia wa Marekani kujiweka tayari
Lakini kana kwamba alikuwa amejitayarisha kwa athari zitakazotokea, Trump tayari amewatahadharisha Wamarekani kujiandaa kwa madhara yatakayoletwa na vita vya kibiashara vitakavyozuka kutokana na ushuru huo.
Wachambuzi wa Taasisi ya Kiuchumi ya Oxford wanakadiria kuwa ushuru huo unaweza kusababisha mfumuko wa bei nchini Mexico kufikia asilimia 6 kila mwaka, kutoka asilimia 4.2 mnamo Desemba, huku sarafu yake ikitarajiwa kushuka kwa asilimia 7. Vilevile, mchumi mkuu wa Taasisi ya Kimataifa ya Tafiti za Uchumi ya EY-Parthenon, Gregory Daco, anabainisha kuwa uchumi wa Canada unaweza kushuka kwa asilimia 2.7 mwaka huu na asilimia 4.3 ifikapo mwaka ujao.
Serikali ya Mexico tayari imetangaza kuwa itawasilisha madai yake kwa Shirika la Biashara Duniani (WTO) dhidi ya Marekani, huku Rais Claudia Sheinbaum akitangaza hatua za kulipiza kisasi kwa bidhaa za Marekani. Wizara ya Biashara ya China, kwa upande wake, imesema kuwa Beijing itachukua hatua zinazolingana na uamuzi huo wa Trump.
Athari za tangazo hili la ushuru tayari zimeanza kuonekana katika masoko ya fedha, likisababisha kushuka kwa zaidi ya asilimia mbili katika masoko ya hisa ya Wall Street, Tokyo, Seoul na Jakarta, huku Bangkok na Wellington zikishuka kwa zaidi ya asilimia moja. Masoko ya Ulaya, ikiwemo London, Paris, na Frankfurt, pia yamekumbwa na mtikisiko tangu yalipofunguliwa mapema leo.