Athari za ukataji misaada wa Marekani kwa Uganda
28 Januari 2025Aidha wakimbizi nchini humo ambao wamekuwa wakipokea misaada mbalimbali kupitia mipango ya shirika la misaada la Marekani USAID nao wanahofia kwamba hali yao ya maisha itaathirika pakubwa kutokana na hatua hiyo iliyoagizwa kuanza kutekelezwa mara moja na serikali ya Marekani.
Kwa mujibu wa ilani iliyosambazwa na shirika la misaada la Marekani USAID kwa mashirika na wadau mbalimbali wanategemea ufadhili kutoka Marekani, hakuna fedha zitasambazwa kwao kuendeleza shughuli za mipango yao na shirika haloitawajibika kugharamia matumizi na malipo yoyote katika kipindi hicho.
Hii imeleta mashaka makubwa hasa katika sekta ya afya ambapo mipango ya huduma kwa watu walio na virusi vya UKIMWI wapatao zaidi ya milioni moja laki mbili imekuwa ikifadhiliwa na USAID.
Kila mwaka, wizara ya afya ya Uganda imekuwa ikipokea dola milioni 471 za Kimarekani ambapo kati ya hizo 426 hufadhili mipango hiyo.
Soma pia:UN: Mamilioni ya watu waathiriwa na njaa kusini mwa Afrika
Aidha takwimu hizo zilizotolewa na ubalozi wa Marekani zinaonyesha kuwa mipango maalum ya afya ya akili iliyotengewa dola bilioni moja kwa miaka mitatu kuanzia mwaka jana nayo itaathirika.
Katibu wa kudumu katika wizara ya Afya Diana Atwine amethibitisha kupokea ilani husika akafafanua kuwa wanajadiliana na USAID kuhakikisha kuwa shughuli nyeti za mipango ya afya zinapata ufadhili kutoka kwa serikali au wadau wengine wa maendeleo.
"Ndiyo wabia wetu wamewasiliana kwa mujibu wa agizo rasmi la rais wa Marekani kwamba wanasitisha ufadhili hadi pale utakapochunguzwa upya lakini tutashauriana nao kuona njia za kuendelea kufadhili shughuli nyeti." Alisema
Mpango wa chakula kuathirika?
Kupitia shirika la mpango wa chakula duniani WFP, Marekani hufadhili mipango ya lishe na chakula kwa kiasi cha dola milioni 82 hasa kwa jamii ya Karamoja ambako idadi kubwa ya watoto hutatizwa na utapiamlo.
Jumuiya nyingine ambayo imeathrika kutoka na kusitishwa kwa misaada hii ni ile ya wakimbizi. Uganda ina wakimbizi zaidi ya milioni moja laki saba na Marekani hutoa angalau dola milioni 100 kila mwaka kugharamia chakula na uwezeshaji wao kujikimu kimaisha kupitia mipango ya elimu,mafunzo na ujasiriamali.
Kwa mfano chini ya mpango ujulikanao kama ‘Uthabiti' wakimbizi wameweza kupokea mtaji kushiriki biashara ndogondogo na pia mashine, pembejeo za kilimo na vifaa mbalimbali.
Soma piaNjia za ardhini kote barani Afrika ni hatari kwa wahamiaji kama safari za Mediterania.:
Arthur Musombwa ni mmoja kati ya viongozi wa wakimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo alisema "bila shaka hali hii imeturudisha nyuma katika harakati zetu za kuboresha maisha yetu kama wakimbizi naomba walegeze kidogo masharti ili tuendelee na mipango" yetu
Hivi karibuni shirika la USAID lilianzisha pia mpango wa kufadhili sekta kwa kiasi cha dola milioni 800 lengo likiwa kuwawezesha kuimarisha uzalishaji wao wanapopanua biashara zao na kuzidisha fursa za kazi na mapato kwa vijana na jamii zinazozalisha mazao vijijini.
Asasi za kiraia kuathirika pia
Mpango huu sasa umekwama. Kwa upande mwingine, asasi kadhaa za kiraia na mashirika yasiyo ya serikali hupokea dola milioni 20 kutoka serikali ya Marekani.
Taasisi hizo hutoa fursa za kazi kwa watu wengi lakini ghafla wamejikuta mashakani kwani hata mishahara yao ya mwezi huu itakuwa shida kulipwa.
Yona Wanjala ni Mkurugenzi Mkuu wa shirika linalotoa ushauri kwa asasi za kiraia alisema wanapata mashaka na tayari wamekwisha azimio kupunguza idadi ya wafanyakazi na kukata matumizi mengine ya uendeshaji wa shughuli zao.
Soma pia:Kwanini migogoro kadhaa ya kibinaadamu imesahaulika Afrika?
Kwa mujibu wa agizo hilo rasmi ambalo rais Donald Trump wa Marekani,ni mataifa ya Misri na Isreal tu ambayo hayaathirika.
Siku ya Jumatatu rais Museveni wa Uganda alikutana na Balozi wa Marekani na kulingana na ujumbe wake kwenye jukwaa la X kwamba waliangazia masuala nyeti ya kimaslahi.
Lakini umma unadhani kuwa suala la misaada ya Marekani kwa Uganda lilijadiliwa kwani nchi hiyo kutoa kiasi cha dola bilioni moja na nusu kila mwaka kusaidia mipango mbalimbali. Lubega Emmanuel DW Kampala.