1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Athari zinazotokana na mzozo wa fedha duniani

Othman, Miraji17 Oktoba 2008

Kila mmoja anaugua kutokana na mzozo wa fedha wa kimataifa

Waziri wa uchumi wa Ujerumani, Michael Glos(kushoto), na mwenzake wa fedha, Peer Steinbrück, wakishauriana bungeniPicha: AP

Athari zilizidi kujitokeza leo kutokana na mzozo wa taasisi za fedha na mabenki ulioikumba dunia hivi sasa, huku watu wakipoteza nafasi zao za kazi na wakuu wa mabenki wakilaumiwa kutokana na kuporomoka bei za hisa za mabenki masokoni. Pia leo mabaraza yote mawili ya bunge la Ujerumani yaliupitisha mpango wa serekali wa kutoa dola bilioni 650 ili kuyanusuru mabenki yasifilisike. Hiyo ni hatua ya kihistoria kutaka kurejesha imani ya wawekezaji katika mabenki na mifumo ya fedha.

Bei za hisa hapa Ulaya na Asia zilipanda juu kidogo mwanzoni mwa siku ya leo, kuigiza hali iliotokea New York na Tokyo, lakini zilikwenda chini baadae pale benki moja nchini Ufaransa ilipokiri kwamba imepata hasara ya dola milioni 800 katika mtafaruku wa sasa wa mabenki. Dalali mmoja wa hisa alinun'gunika na kusema amechoshwa na hali ya sasa ya bei mara kwenda juu sana na mara kushuka chini sana. Alisema anahitaji mapumziko kidogo ya hali hiyo.

Nayo Ukraine ilisema ilikuwa inashauriana na Shirika la Fedha la Kitaifa, IMF, kupatiwa mkopo wa dharura, huku Argentina ikitangaza imeafikiana na mabenki matatu ya kigeni ili kufanya mashauriano mepya kuhusu malipo ya kila mwaka ya sehemu ya mrundiko wa mkopo wake wa dola bilioni 150. Makampuni zaidi duniani yanalaumu kwamba hali ya sasa ya kupotea nafasi za kazi inatokana na mzozo huu wa sasa ambapo mabenki yamezuwia kutoa mikopo kwa wafanya biashara kutokana na hasara iliopatikana hapo awali kutokana na mikopo ya kununulia majumba nchini Marekani.

Kampuni ya Kichina ya kutengeneza vitu vya kuchezea watoto, ambayo ilikuwa inategemea ruwaza ya vitu vinavotengenezwa na kampuni za Kimarekani, kama vile Mattel na Disney, imefilisika kutokana na mzozo huu wa sasa, hivyo watu 7,000 kupoteza kazi. Kampuni hiyo ilifunga kiwanda chake wiki hii, wafanya kazi ambao walikosa kulipwa mishahara yao walibakia wameduwaa na kusimama nje ya milango ya kiwanda hicho. Kampuni ya Sweden ya kutengeneza magari ya aina ya Saab ilisema itapunguza wafanya kazi 500 mnamo miaka miwili baada ya kutangaza kwamba imepata hasara kubwa. Ukosefu wa kazi umezidi hapa Ulaya, sekta muhimu kama vile ya kutengeneza magari ikiumia zaidi.

Josef Ackermann, mkuu wa benki kubwa kabisa hapa Ujerumani, Deutsche Bank, amesema hatachukuwa marupurupu yake ya kila mwaka ya mamilioni kadhaa ya Euro; hii ni kuonesha mashikamano yake na wafanya kazi wa benki hiyo. Hapa Ulaya wananchi wengi hawafurahishwi na malipo makubwa wanayopewa mameneja wa mabenki, wakidaiwa kwamba wao pia wanabeba dhamana ya hali ya sasa ilio ngumu katika mabenki.

Na mpango mkubwa kabisa wa kuuokoa uchumi kuwahi kusukwa hapa Ujerumani baada ya vita vikuu vya pili vya dunia, leo ulikubaliwa na mabaraza yote mawili ya bunge. Ulikubaliwa kwa kauli moja na baraza la mikoa na hapo mwanzo asubuhi wabunge 476 waliuunga mkono , 99 kuupinga na mbunge moja hajapigia kura upande wowote. Baadae mpango huo wenye kugharimu Euro 480 zitakazotengwa kwa ajili ya kuyasaidia mabenki ulipata saini ya mwisho ya Rais Horst Köhler.

Waziri wa uchumi, Michael Glos, alisema mpango huo ni muhimu sana sio tu kwa mabenki, lakini hasa kwa maslahi ya raia na uchumi. Alisema mpango huo hauna maana ya kuyataifisha mabenki:

"Sekta ya mabenki inayodhibitiwa na dola ni jambo ambalo kwangu mimi lina sura ya kutisha."

Hadi sasa hamna benki iliotoa ishara ya kuwa na nia ya kuomba msaada huo, Na kwa mujibu wa makisio ya serekali uchumi wa Ujerumani utapanda kwa asilimia 0.2 hapo mwakani, kiwango cha chini kabisa kuwahi kushuhudiwa tangu uchumi kwenda chini mwaka 2002-2003. Lakini waziri wa fedha, Peer Steinbrück , amesema uchumi wa Ujerumani ni imara vya kutosha kuweza kuhimili hali ya sasa ya uchumi wa dunia kupwaya.




Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW