Atletico Madrid yaiadhibu Barcelona bao 2-0
9 Aprili 2026
Atletico Madrid ilipata ushindi muhimu wa 2-0 dhidi ya Barcelona ugenini baada ya wapinzani wao kubaki na wachezaji 10 katika mechi ya robo fainali ya Ligi ya mabingwa Ulaya, Champions League.
Barcelona ilikuwa ikitawala mchezo na kuibana Atletico, lakini mambo yalibadilika ghafla kabla ya mapumziko baada ya beki Pau Cubarsí kuoneshwa kadi nyekundu kufuatia faulo dhidi ya Giuliano Simeone aliyekuwa anaelekea golini.
Baada ya kadi hiyo, Barcelona ilipata pigo la pili mara moja ambapo Julián Álvarez aliifungia Atletico bao la kwanza kupitia mkwaju wa faulo uliopita juu ya ukuta wa walinzi na kumshinda kipa Joan García katika dakika ya 45.
Bao hilo liliipa Atletico morali kubwa huku Barcelona ikilazimika kucheza nusu ya pili ikiwa pungufu kwa idadi ya wachezaji.
Licha ya juhudi za Lamine Yamal na Marcus Rashford kuisukuma Barcelona kusawazisha, Atletico ilidhibiti mchezo vizuri.
Dakika 20 kabla ya kipenga cha kumaliza mchezo, Alexander Sorloth aliyekuwa ametokea benchi alifunga bao la pili kwa kumalizia krosi ya Matteo Ruggeri, na kuihakikishia Atletico nguvu zaidi kuelekea mchezo wa marudiano wa robo fainali utakaochezwa Madrid Jumanne ijayo.