AU na mgogoro wa Comoro
21 Februari 2008Uamuzi huo umefikiwa katika kikao cha umoja wa Afrika cha kundi la nchi zilizopewa jukumu la kuwasiliana na pande zinazohusika katika mgogoro huo wa Nzuwani. Nchi hizo ni Tanzania, Libya, Senegal na Sudan.
Akizungumza na waandishi habari baada ya mkutano wa mawaziri wa kundi hilo, Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Tanzania Bernard Kamillius Membe ambaye alikua mwenyekiti wa pamoja na kamishna wa umoja huo anayehusika na amani na usalama Said Djinnit, alisema kwamba, umoja wa Afrika uameamua kuisaidia serikali ya Comoro ya Rais Ahmed Abdullah Sambi kijeshi na mbinu kati ya sasa na tarehe 30 mwezi ujao wa Machi ili kurejesha amani na utulivu kisiwani Nzuwani haraka iwezekanavyo.
Umoja huo umeamua pia kutuma mara moja Comoro kikundi cha kutathimini mahitaji ya kijeshi na usalama pamoja na kikundi cha maandalizi kukamilisha hataua hiyo.
Tarehe 31 Januari Rais Sambi akivunjwa na kile alichosema ni kushindwa kwa umoja wa Afrika kuchukua hatua dhidi ya uasi unaoendelea wa Kanali Bakari huko Nzuwani, alitangaza azama yake ya kutumia nguvu za kijeshi kulinda mamlaka, uhuru na umoja wa visiwa hivyo. Sambi akayasisitiza hayo wakati akihutubia kikao cha 10 cha viongozi wakuu wa umoja wa Afrika mjini Addis Ababa.
Kisiwa cha Nzuwani kimo kwenye mgogoro na serikali kuu ya Comoro tangu Juni 10 mwaka jana baada ya Kanali Bakari kuitisha uchaguzi kimabavu kinyume na matakwa ya serikali ya umoja wa visiwa hivyo, ikishikilia kubakia madarakani.
Uamuzi wa umoja wa Afrika hivi kuiunga mkono serikali kuu kijeshi, umeungwa mkono paia na Ufaransa mtawala wa zamani awa visiawa hivyo, ambayo imesema itasaidia kuwasafirisha wanajeshi wa umoja wa Afrika hadi Comoro. Kwa sasa tayari kuna kiasi ya wanajeshi 300 kutoka Tanzania sehemu ya jeshi la kulinda amani la umoja wa Afrika visiwani humo.
Taarifa zinasema mbali na Tanzania nchi nyengine katika kundi hilo la mawasiliano zimekubali kuchangia pia wanajeshi. Visiwa vya komoro vinaundwa na Ngazija kisiwa kikuu, Nzuwani na Mwali. Kisiwa cha nne bado kimo katika mamlaka ya Ufaransa licha ya kura ya maoni kuunga mkono Uhuru 1974. Visiwa hivyo vilijitangazia uhuru Aprili 6 , 1975. tangu wakati huo vimekubwa na mapinduzi kadhaa, njama za mapinduzi na migogoro ya kisiasa.