AU yaidhinisha mkakati wa kujitoa katika ICC
1 Februari 2017Viongozi hao wa Umoja wa Afrika waliidhinisha pendekezo hilo wakati wakikaribia kumaliza mkutano wao wa kilele wa siku mbili hapo jana mjini Addis Ababa. Uamuzi wao unaashiria msimamo wa viongozi wa kiafrika wa kutokuwa tena na uvumilifu kuhusu utendaji wa Mahakama hiyo ya Kimataifa-ICC, ambapo baadhi wanadai kwamba imekuwa tu ikiziandama zaidi nchi za kiafrika na kuendesha kesi zinazohusiana na mauaji ya kimbari, uhalifu wa kivita na maovu mengine dhidi ya binaadamu na kushindwa kuchukua hatua kuhusiana na matukio ya aina hiyo kwengineko nje ya bara hilo.
Mnamo mwaka uliopita Afrika Kusini, Burundi na Gambia zilitangaza nia ya kujitoa katika mahakama hiyo, na kuzusha wasiwasi kwamba huenda nchi nyengine zikafuata. Mkuu wa ofisi ya Shirika la Kimataifa la misaada Oxfam katika Umoja wa Afrika Desire Assogbavi, alithibitisha kuidhinishwa kwa mkakati huo.
Duru moja katika baraza la sheria la umoja huo ambayo haikutaka kutajwa jina kwa kuwa hairuhusiwi kuzungumza na vyombo vya habari ilisema nchi wanachama ziligawika ilipozuka hoja iwapo zitowe wito wa kujitoa katika mahakama hiyo ya mjini The Hague kwa pamoja au kila nchi peke yake.
Baadhi ya nchi za Kiafrika zimekuwa zikiikosoa ICC kwa kuwaandama viongozi wa taifa barani Afrika. Kwa mfano Rais Omar Hassan al-Bashir wa Sudan amekuwa akisakwa na mahakama hiyo tangu 2009, kwa madai ya kupanga mauaji katika jimbo la magharibi mwa Sudan la Darfur.
Mahakama hiyo ya kimataifa pia ilisababisha mzozo na mabishano na baadhi ya mataifa ya Kiafrika, baada ya kumfungulia mashtaka ya uhalifu na maovu dhidi ya binaadamu Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya , kufuatia machafuko yaliotokea kufuatia uchaguzi wa 2007 ambapo zaidi ya watu 1,000 waliuwawa. Kesi hiyo ilishindwa baada ya mwendesha mashtaka wa ICC kusema ameshindwa kupata ushirikiano kutoka serikali ya Kenya . Swali hivi sasa ni iwapo nchi za kiafrika kweli zitakuwa na ubavu wa kujitoa kwa pamoja na athari za hatua hiyo. Bw Agina Ojwang ni mwanasheria na mchambuzi wa masuala ya ICC, aliyeko mjini Nairobi.
Afisa anayehusika na mpango wa sheria katika Shirika la Haki za Binaadamu Human Rights watch Elise Keppler amesema mkakati wa kujitoa katika Mahakama ya ICC, hakuna muda maalum na mapendekezo madhubuti kuhusu hatua hiyo ni machache mno. Alisema mnamo miezi ya hivi karibuni nchi kadhaa za Kiafrika zikiwemo Nigeria, Senegal na Congo, zimekuwa zikielezea misimamo yao, zikiiunga mkono Mahakama hiyo.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Associated Press, waraka wa mkakati huo wa pamoja wa nchi za kiafrika kujitoa katika Mahakama ya uhalifu ya kimataifa ICC, umependekeza badala yake nchi hizo ziimarishe mifumo yao yenyewe ya kisheria na kutanua uwezo wa kiutendaji wa Mahakama ya Sheria na Haki za Binaadamu ya Afrika, ili kupunguza kuitegemea Mahakama ya Kimataifa -ICC
Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman, dpa, ap
Mhariri: Iddi Ssessanga