1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaEthiopia

AU yakutana lakini maswali kuhusu uwezo wake ni mengi

13 Februari 2026

ICG: Wakati Umoja wa Afrika unahitajika zaidi kuchukua hatua, inaweza kusemwa kuwa huwa unapatikana ukiwa dhaifu zaidi tangu kuasisiwa kwake.

Ethiopia Addis Abeba 2025 | Mkutano wa 38 wa Umoja wa Afrika
Umoja wa Afrika-AU umelazimika kupuuza sheria yake inayozuia viongozi wa mapinduzi kuwania uongozi kwenye uchaguzi.Picha: Solomon Muchie/DW

Umoja wa Afrika utafanya mkutano wake wa kilele mwisho wa juma hili nchini Ethiopia, mnamo wakati visa vya mauaji ya halaiki, mashambulizi ya wanamgambo na mapinduzi ya serikali vikizidi kulizonga bara hilo, lakini bila ya masuluhisho thabiti ya kutosha. 

Mapinduzi, migogoro na ukiukaji wa haki ni miongoni mwa mambo yanayotarajiwa kuwa kwenye ajenda ya mkutano huo, lakini mada kuu ni usafi wa maji.

Umoja wa Afrika-AU uliundwa mwaka 2002 na una wanachama 55 ambao mara kwa mara hukinzana katika masuala mengi.

Mara nyingi, nchi wanachama zimezuia majaribio ya kuupa umoja huo nguvu kamili ya utekelezaji kuweza kudhibiti hatua zao, hali ambayo imeuacha umoja huo ikiwa na ufadhili mdogo na bila ya vifaa muhimu vinavyohitajika.

Umoja usioweza kujifadhili na kujitegemea kikamilifu

Majaribio yake ya kujifadhili na kujitegemea, yamegonga mwamba ikiwemo mwaka 2020 na 2025. Hadi sasa, Umoja wa Afrika unategemea asilimia 64 ya bajeti yake ya kila mwaka kufadhiliwa kwa misaada ya Marekani na Umoja wa Ulaya, ambazo kwa sasa zinapunguza misaada yao.

Machafuko yanayozonga baadhi ya nchi Afrika ikiwemo Sudan ni miongoni mwa masuala ambayo Umoja wa Afrika umeshindwa kusuluhishaPicha: El Tayeb Siddig/REUTERS

Mwenyekiti wa halmashauri kuu ya umoja huo Ali Youssouf amebaki kuelezea tu wasiwasi mkubwa kuhusu migogoro isiyoisha inayozonga bara lake, ikiwemo vita nchini Sudan na katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, mashambulizi ya wanamgambo katika kanda ya Sahel, lakini bila ya uwezo wa kuchukua hatua madhubuti kuvikomesha.

Shirika la Kimataifa linaloshughulikia Migogoro (ICG), katika ripoti yake ya hivi karibuni ilisema wakati Umoja wa Afrika unahitajika zaidi kuchukua hatua, inaweza kusemwa kuwa huwa unapatikana ukiwa dhaifu zaidi tangu kuasisiwa kwake.

Umoja unaovunja sheria zake yenyewe

Huku kukiwa na mapinduzi 10 ya kijeshi barani Afrika tangu 2020, AU imelazimika kupuuza sheria yake kwamba viongozi wa mapinduzi hawapaswi kuwania uchaguzi.

Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika Ali Youssouf Picha: Amanuel Sileshi/AFP/Getty Images

Gabon na Guinea ziliondolewa katika umoja huo baada ya mapinduzi, lakini zilirejeshwa mwaka uliopita ndani ya umoja huo, licha ya kuvunja sheria hiyo.

Aidha hakujakuwa na matamko mazito ya kuelezea kusikitishwa mno na chaguzi kadhaa ambazo zimegubikwa na udanganyifu na machafuko makubwa miongoni mwa nchi wanachama. 

Katika mkutano wa mwisho wa wiki, rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye, anatarajiwa kuchukua uongozi wa kupokezana wa umoja huo.

Umoja unaosifia maovu badala ya kulaani?

Mnamo Oktoba mwaka uliopita, Youssouf alikuwa mwepesi katika kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan baada ya kupata ushindi wa asilimia 98 katika uchaguzi wa rais nchini Tanzania. Uchaguzi ambao washindani wake wote wakuu walizuiwa au walikuwa gerezani. Isitoshe vikosi vya usalama vilituhumiwa kuwaua maelfu ya waandamanaji.

Umoja wa Afrika ulisifia ushindi wa asilimia 98 wa Rais Samia SUluhu Hassan katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, licha ya uchaguzi huo kukumbwa na maafa ya waandamanaji.Picha: Thomas Mukoya/REUTERS

Umoja wa Afrika pia ulisifia kile ulichokitaja kuwa uwazi katika uchaguzi wa Burundi, lakini ambao waangalizi wa Haki za Binadamu walitaja kujaa ukandamizaji.

Benjamin Auge kutoka Taasisi ya Ufaransa kuhusu Uhusiano wa Kimataifa amehoji kuwa tatizo lililopo ni kwamba viongozi wachache wa Afrika ndio hujali jinsi ulimwengu wa nje unavyowatizama tofauti na hali ilivyokuwa miaka ya awali baada ya uhuru, na kwamba hakuna marais wengi wenye malengo yanayokuza mshikamano, umoja, na ushirikiano wa kiuchumi na kisiasa miongoni mwa watu wote wenye asili ya Kiafrika, barani Afrika kwenyewe na walio nje ya nchi.

Akizungumza na shirika la habari la AFP, Auge amesema viongozi wengi wa Afrika wanashughulika zaidi na matatizo yao ya ndani na hawashughuliki zaidi na masuala ya Umoja wa Afrika.

(AFPE)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW