1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zaidi ya wahamiaji 40 wauawa Libya

Angela Mdungu
3 Julai 2019

Zaidi ya wahamiaji 30 wameuawa mapema hii leo na takribani 80 wamejeruhiwa baada ya ndege kushambulia kituo walichokuwa wakishikiliwa wahamiaji hao mjini Tripoli nchini Libya

Luftangriff auf Gaza Stadt
Picha: Reuters

Msemaji wa shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa, ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba kituo kilichoshambuliwa kilikuwa kikiwashikilia wahamiaji 600 na kwamba pamoja na uwepo wa timu ya madaktari wanaowahudumia watu waliojeruhiwa huenda idadi ya vifo ikaongezeka.

Ingawa bado hakuna kundi lililojitangaza kutekeleza tukio hilo, vikosi vya Jenerali muasi Khalifa Haftar, vinanyooshewa kidole na vikosi vya serikali ya Libya kuhusika na shambulizi hilo lililolenga kituo hicho chenye zaidi makazi 120 ya wahamiaji nje kidogo mwa mji mkuuTripoli.  Jenerali huyo anayedhibiti sehemu kubwa ya Mashariki na Kusini mwa Libya, amekuwa akipigana na vikosi vya jeshi la serikali inayotambuliwa kimataifa ya Libya na amekuwa akijaribu kupata udhibiti wa mji mkuu wa nchi hiyo.

Vituo vingi vinamilikiwa na makundi ya wanamgambo

Wahamiaji wengi wakimbizi wanaoshikiliwa katika vituo mbalimbali nchini Libya ni raia wa nchi za Eritrea, Ethiopia, Somalia na Sudan. Vituo hivyo vinamilikiwa na makundi ya wanamgambo ambao wanadaiwa kuwadhalilisha wahamiaji hao na kuwatesa na vina kiasi kidogo cha chakula, na ukosefu wa mahitaji muhimu kwa wahamiaji.

Wahamiaji wakitafakari baada ya shambulizi la anga mjini LibyaPicha: Getty Images/AFP/M. Turkia

Wengi wa wakimbizi hao huishia nchini humo katika harakati za kutaka kukimbilia kwenye nchi za ulaya kupitia bahari ya Mediterania. Kwa mujibu wa shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa zaidi ya wahamiaji  3,000 wako hatarini kutokana na kushikiliwa kwa wakimbizi hao na wanamgambo wenye uhusiano na Haftar pamoja na wanamgambo wanaoshirikiana na vikosi vya serikali ya Libya.

Kufuatia tukio la kushambuliwa kituo wanachoshikiliwa wahamiaji, Umoja wa nchi za Afrika, AU umelaani vikali shambulio hilo na kutaka waliohusika kulitekeleza wakamatwe mara moja. Katika taarifa yake, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Afrika, Moussa Faki Mahmat, amesema kuna haja ya kufanyika kwa uchunguzi huru ili kuhakikisha kuwa waliotekeleza shambulizi lililochukua uhai wa raia wasio na hatia wanafikishwa mbele ya vyombo vya sheria.

Mahmat amezitaka pia pande zinazohasimiana nchini Libya kuweka silaha chini, na kuhakikisha usalama wa raia wote ukiwemo wa wahamiaji wanaoshikiliwa katika vituo maalumu. Umoja wa nchi za Afrika, pia umetoa pia wito kwa jumuiya ya kimataifa kuongeza juhudi katika kuzileta pande zinazotofautiana nchini humo katika meza ya mazungumzo.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW