1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AU yataka DRC isitishe kutoa matokeo rasmi ya uchaguzi

Sylvia Mwehozi
18 Januari 2019

Umoja wa Afrika umeitolea mwito Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuahirisha utoaji wa matokeo rasmi ya uchaguzi wa rais ambayo bado yanazozaniwa, kutokana na kuwepo na wasiwasi juu ya matokeo ya awali.

Äthiopien Addis Abeba Moussa Faki
Picha: picture-alliance/AA/M. W. Hailu

Umoja huo uliokutana siku ya Alhamis katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, ulihitimisha kwamba kulikuwa na "wasiwasi mkubwa katika ulinganifu wa matokeo ya awali, kama yalivyAotolewa na tume huru ya uchaguzi". Mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat  amesema kuwa, "hata hivyo, ingawa hali nchini humo imebaki kuwa tulivu hadi sasa, lakini inatia shaka. Ili kuliweka wazi, ni kwamba wasiwasi mkubwa juu ya ulinganifu wa matokeo yaliyotangazwa, yanaendelea kugonga vichwa vya wacongomani na ndugu zao wote kote duniani," alisema Mahamat.

Hoja hiyo ya nadra kutoka Umoja wa Afrika inaibua wasiwasi mpya katika mchakato wa baada ya uchaguzi, ambao ulikuwa na maana ya kulivusha taifa hilo kwa mara ya kwanza katika kukabidhiana madaraka kidemokrasia ndani ya miaka 59 ya uhuru, lakini limejikuta katika mkwamo tangu kura ya Desemba 30.

Matokeo rasmi yanatarajiwa kutolewa na tume ya uchaguzi siku ya Ijumaa mara baada ya mahakama ya katiba kutolea uamuzi changamoto zilizowasilishwa baada ya matokeo ya awali kutangazwa. Lakini Umoja wa Afrika unataka matokeo rasmi yasitangazwe kufuatia wasiwasi uliopo.

Felix Tshisekedi mgombea aliyetangazwa kushinda uchaguzi wa rais Congo Picha: Reuters/O. Acland

Msemaji wa serikali ya Congo Lambert Mende amelaani kauli hiyo ya Umoja wa Afrika akisema mahakama inayochunguza uhalali wa kura ilikuwa "huru". "Sidhani ni wajibu a serikali au Umoja wa Afrika kuieleza mahakama ya katiba nini cha kufanya".

Vyombo vya habari kadhaa vya kimataifa siku ya Jumanne wiki hii viliripoti kwamba taarifa za kura zilizovuja zilionyesha mgombea wa upinzani Martin Fayulu ndiye aliyeshinda katika uchaguzi uliofanyika Desemba 30. Kituo cha utangazaji cha Ufaransa RFI, gazeti la Uingereza la Financial Times na televisheni ya TV5 Monte, ziliripoti kwamba data za kura zilizovuja, ambazo hazichapishwa zinaonyesha mgombea aliyetangazwa na tume ya uchaguzi Felix Tshisekedi hakushinda.

Fayulu alidai kulikuwa na udanganyifu na tayari amepeleka shauri kwenye mahakama ya juu akitaka kura zihesabiwe upya. Anapendekeza kwamba Tshisekedi na rais Joseph Kabila walifikia makubaliano baada ya matokeo ya awali kuonyesha mgombea kutoka chama tawala Emmanuel Ramazani Shadary aliibuka nafasi ya tatu.

Mapema jana Jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika SADC iliondoa shinikizo lake dhidi ya mamlaka ya Congo ambapo awali iliunga mkono wito wa kura kuhesabiwa tena.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/dpa/Reuters

Mhariri: Saumu Yusuf

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW